Sunday, April 19, 2015

Mwanamke akiri kuanzisha danguro la wasichana Dar



Mwanamke akiri kuanzisha danguro la wasichana Dar
 Ni biashara ya ngono ikiwamo ya jinsia moja ,Wasichana wazungumza suluba wanazopata
Mwanamke mmoja, mkazi wa Mabibo Mwisho, jijini Dar es Salaam, anadaiwa kuanzisha danguro la wasichana na kuendesha biashara ya ngono ikiwamo ya jinsia moja.

Mwanamke huyo anayefahamika kwa jina la mama Uzuri, anadaiwa kuwachukua wasichana hao kutoka vijijini kwa kuwadanganya kuwa anakwenda kuwatafutia kazi mjini.

Inadaiwa kuwa fedha anazopata kutokana na biashara hiyo, huzitumia kama gharama ya kuwatunza wasichana hao.

Wakizungumza Jumapili kwa nyakati tofauti, wasichana hao (majina yanahifadhiwa), walidai kuwa mwanamke huyo aliwachukua vijijini kwao kwa ahadi ya ajira za ndani.

Wakielezea undani wa biashara hiyo, walisema wanaume wengi wamekuwa wakiwalazimisha kufanya mapenzi bila kinga (kondom), kwa madai kuwa kwa kufanya hivyo kunawanyima starehe ya tendo hilo.

Suzana (sio jina lake halisi), alisema makazi yao ni nyumbani kwa mwanamke huyo ambapo hulelewa katika mazingira mazuri, na kati yao kuna makahaba na wasagaji.

Alisema, mwanzo walipoanza biashara hiyo walipata wakati mgumu lakini kadiri siku zinavyokwenda waliizoea.

Alisema baadhi yao wanachukuliwa na wanaume zaidi ya mmoja  kwa siku na wakati mwingine hugeuka kuwa walimu kwa wasichana wapya wanaoletwa kutoka vijijini.

"Wakati nachukuliwa kwa wazazi wangu, mwajiri wangu aliwaeleza kwamba nakuja kufanya kazi za ndani kwa ndugu yake, na kamwe sitopata madhara yoyote kutokana na ulinzi na usimamizi nitakaoandaliwa, lakini baada ya kufika hali ikawa tofauti," alisema na kuongeza:

"Nilipokelewa vizuri na wasichana wenzangu niliowakuta, lakini nilishangazwa na kauli ya mwajiri wangu kuwa nahitaji kufanyiwa ukarabati wa kutosha, na akatoa agizo kutofanyishwa kazi yoyote badala yake nipumzike na nitaandaliwa kila kitu ninachokitaka, lakini atakaponituma sehemu na wenzangu nikatekeleze kama atakavyoniagiza, alisema Suzana.

Uchunguzi wetu katika mahojiano na mwanamke huyo, alisema ni vigumu kuiacha biashara hiyo kwa sababu aliianzisha siku nyingi akiwa na wasichana watano.

Alisema wasichana hao amewaajiri kwa gharama kutokana na shughuli wanazozifanya, na  wanapokwenda kijijini kwa wazazi wao, huwagharamia matumizi na zawadi kwa familia zao.

Alisema gharama za biashara hiyo hutofautiana kulingana na kiwango cha mteja, lakini kwa wale wanaofanyiwa tendo hilo kinyume na maumbile, wateja hutozwa Sh. 20,000, na ngono ya kawaida Sh. 5,000 hadi  Sh.10,000 kwa mara moja.

Aidha, alisema wanaofanya tendo hilo kwa jinsia moja (wasagaji), gharama zake hazitofautiani.

 "Kifupi wasichana wangu wanajituma hata wateja wenyewe wanawakubali ndani na nje ya Dar es Salaam, lakini biashara ina msimu, kuna wakati inakulipa na wakati mwingine inasuasua.

"Kikubwa ni ujanja na namna ya kuwaandaa wasichana, kwa bahati nzuri katika familia zao hakuna anayejua kazi anayoifanya mtoto wake zaidi ya 'house girl'. Ni marufuku kutoa siri ya kazi hivyo ni lazima niwekeze kwao kwa gharama yoyote maana najua wanachokifanya mjini," alijitapa mwanamke huyo.

Alisema ingawa anajua kuna maradhi lakini amekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwao ili waweze kujikinga na magonjwa hatari yanayoenezwa kwa njia ya ngono pamoja na ugonjwa hatari wa Ukimwi.