HATIMAYE siri za kifo chenye utata cha msanii maarufu wa filamu
nchini, Steven Charles Kanumba (28), kilichotokea usiku wa kuamkia juzi
nyumbani kwake Sinza Vatcan jijini Dar es Salaam zimeanza kufichuka.
Kanumba aliyefariki ghafla baada ya kudaiwa kuanguka akiwa ndani
kwake na mpenzi wake, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu (18), taarifa
za kifo chake zimekuwa na mkanganyiko ambapo baadhi ya watu wanadai
kuwa alinyweshwa sumu na wengine wakisema alipigwa na kitu chenye ncha
kali kisogoni.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, jana lilitoa taarifa ya
uchunguzi wa awali likisema kuwa mbali na maelezo ya mdogo wa marehemu,
Seth Bosco (24), pia panga, pombe aina ya ‘whisky’ ikiwa robo glasi na
soda aina ya sprite vilionekana chumbani kwake.
Kamanda Kenyela alisema kuwa vinywaji hivyo vitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo na uchunguzi zaidi.
Alipoulizwa kama marehemu Kanumba alikuwa amekunywa pombe siku hiyo,
Kamanda Kenyela alisema ni vigumu kubaini hilo ila ukweli wake
utajulikana kwenye uchunguzi wa mwili wake (postmortem).
Akifafanua zaidi kuhusu chanzo cha kifo cha Kanumba, Kamanda Kenyela
alisema kwa mujibu wa mdogo wake, Bosco, ambaye pia ni msanii wa kikundi
cha The Great Filamu Production, siku ya tukio aliambiwa na kaka yake
kuwa ajiandae ili amsindikize sehemu.
Alisema kuwa baada ya kumweleza hivyo, Kanumba aliingia chumbani kwake
kujiandaa na kwamba baada ya muda kidogo alimwita mdogo wake chumbani
kuwa kuna mgeni, ndipo Bosco akamwambia akiwa tayari angemuona.
Kamanda alisema kuwa muda mfupi baadaye Bosco anasema alisikia kelele ambapo kaka yake alikuwa akimtuhumu mpenzi wake Lulu.
Kenyela alisema kuwa Bosco alieleza kwamba alisikia sauti ya Kanumba
akimhoji Lulu: “Kwa nini unawapigia simu mabwana zako wengine?”
Ghafla Bosco aliitwa na msichana huyo na kumuambia kuwa akamwangalie kaka yake amezidiwa.
Bosco alieleza kuwa aliingia chumbani na kumkuta Kanumba amelala sakafuni huku akitokwa na povu mdomoni akiwa haongei.
Alisema kuwa alitoka nje na kumwangalia Lulu, lakini hakumuona na
hivyo kuamua kumpigia simu daktari wa Kanumba ambaye baada ya kufika
aligundua kuwa amekwishafariki.
Kenyela aliongeza kuwa mwili wa marehemu Kanumba haukukutwa na jeraha
lolote na kwamba umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili huku
Lulu ambaye ni mkazi wa Tabata Relini akiendelea kuhojiwa kuhusiana na
tukio hilo.
JK awafariji wafiwa
Rais Jakaya Kikwete, jana alifika nyumbani kwa marehemu Kanumba na
kuwafariji wafiwa, akisema kuwa kifo chake ni pigo kwa taifa kutokana na
juhudi zake alizokuwa amezianza za kuitangaza Tanzania nje katika
tasnia ya filamu.
Rais ambaye alisaini kitabu cha maombolezo na kisha kuzungumza na
ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu nyumbani hapo, alisema kuwa Kanumba
alikuwa ni msanii anayependa maendeleo ya wengine ndiyo maana
alijitolea kuwainua baadhi ya wasanii.
Aliwataka wasanii wenzake kuuenzi utaratibu huo ili nao waje wakumbukwe pindi watakapoondoka katika uso wa dunia.
Rais Kikwete aliwataka wafiwa wawe na subira huku wakiendelea kumuomba
Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kukabiliana na hali ngumu waliyonayo ya
kuomdokewa na kipenzi chao.
Naye, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, leo saa tatu asubuhi anatarajiwa
kuwasili nyumbani kwa marehemu Kunumba kuwafariji wafiwa kisha ataondoka
kuelekea Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge vinavyoanza kesho.
CUF watuma rambirambi
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kuwa kimepokea taarifa ya kifo cha
Kanumba kwa masikitiko makubwa na hivyo kuwataka Watanzania kuungana
kwa pamoja katika kipindi hiki cha majonzi na kumuombea marehemu.
Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki
za Binadamu wa chama hicho, Abdul Kambaya, ilisema kuwa Kanumba ambaye
alikuwa msanii muhimu, pengo lake halitazibika kirahisi katika jamii ya
sanaa.
“Wananchi wote tunaamini kuwa jamii ya wasanii tumepoteza msanii
muhimu ambaye pengo lake halitazibika kirahisi katika jamii yetu, hivyo
CUF inaungana na Watanzania wote kwa kutoa pole kwa familia, ndugu na
jamaa,” alisema.
Kuzikwa kesho
Taarifa iliyotolewa jana jioni na mmoja wa wana kamati ya mazishi,
Hidi Mchome, ilisema kuwa Kanumba atazikwa kesho katika makaburi ya
Kinondoni majira ya alasiri.
Mchome alisema uamuzi huo ni baada ya ndugu zake kuwasili akiwemo mama
yake mzazi na kwamba salamu za mwisho za kuuaga mwili wa marehemu
zitatolewa katika viwanja vya Leaders Club kuanzia saa nne asubuhi.
Mamia wafurika nyumbani
Katika siku ya pili ya maombolezo jana, mamia ya watu wa kada
mbalimbali walifika nyumbani kwa marehemu kuwafariji ndugu na jamaa
zake.
Kutokana na eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya watu, Jeshi la Polisi
Mkoa wa Kinondoni limeimarisha ulinzi wa kutosha ikiwa ni pamoja na
kuifunga kwa muda barabara ya Sinza-Magomeni eneo la Vatican.
Source: Tanzania Daima.
|