Sunday, April 19, 2015

Ripoti ya Escrow yatua kwa JK kutoka Baraza la Maadili



Ripoti ya Escrow yatua kwa JK kutoka Baraza la Maadili
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, limesema limeshawasilisha ripoti yake kwa Rais Jakaya Kikwete, baada ya kumaliza kazi ya kuwahoji viongozi waliokumbwa na kashfa ya Tegeta Escrow.

Kamishna wa Sekretarieti ya Maandili ya Baraza hilo, Jaji Mstaafu, Salome Kaganda, alituambia katika mahojiano maalum juzi kuwa tayari Baraza lake limeshawasilisha ripoti hiyo kwa Rais na kinachosubiriwa ni majibu. 

Waliohojiwa na Baraza hilo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye alipewa mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa Mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira.

Wengine ni Mbunge wa Jimbo la Sengerema na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye alichotewa Sh. million 40 katika mgawo huo.

Katika sakata hilo pia, Afisa wa Ikulu, Shabani Gurumo, alihojiwa baada ya kudaiwa kupokea Sh. milioni 80.

"Tayari nimeshaiwasilisha ripoti nasubiri majibu ila sikumbuki terehe niliyoipeleka," alisema Jaji Kaganda.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, awali alipoulizwa kuhusu hatma ya waliohojiwa, alisema, ameshamaliza kazi yake na kuiwasilisha kwa Kamishna ili ipelekwe kwa Rais.

Alisema haelewi kinachoendelea kwa kuwa yeye hana ofisi.
Jumapili tulizungumza na Katibu Kiongozi Ikulu, Balozi Ombeni Sefue ambaye alisema ripoti hiyo itapitiwa kwa umakini ili kujua hatua zitakazochukuliwa.

Alisema ripoti hiyo pamoja na ripoti ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, zitakwenda pamoja katika maamuzi.

Katika sakata hilo, vigogo watatu waligoma kuhojiwa kwa madai wanakwenda Mahakama Kuu kufungua kesi ya pingamizi.

Vigogo hao ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko na Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo.

Chenge anadaiwa wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa serikali mwaka 1995, aliishauri serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na IPTL. Na baada ya kustaafu, aliingia mkataba kuwa mshauri wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na hisa asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL.
Ilidaiwa kuwa kitendo cha kuingia mkataba huo ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Katika mgawo wa fedha za Tegeta Escrow, Chenge alipokea Sh. bilioni 1.6, ikiwa ni sehemu ya fedha zilizochotwa katika akaunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Saliboko anadaiwa kupokea mgawo wa Sh. milioni 40.4  na Appollo alipokea Sh. milioni 80.8 kutoka kwa Rugemalira, kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.