Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka serikali kuchukua hatua za haraka za kuwarudisha Watanzania waliopo Afrika Kusini, baada ya kuibuka ghasia za kuwashambulia wageni wa kiafrika waishio humo.
Kauli ya Chadema imekuja wakati raia wa nchi hiyo wakiendeleza mashambulizi ya kuwajeruhi na kuwaua wageni kwa kile walichoeleza kuwa wanapora ajira zao.
Mkuu wa Mambo ya Nje wa chama hicho, Deogratias Munishi, katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, ameitaka Tanzania kushirikiana na Afrika Kusini kuwarejesha Watanzania nyumbani au kuwapeleka kwenye miji isiyo na machafuko.
Chadema kimezikumbusha nchi za Afrika ambazo zina utajiri mkubwa wa rasilimali kuhakikisha zinatatua matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo ikiwa ni pamoja na kupunguza tofauti ya kipato.
Aidha, chama hicho kinalaani vikali hali ya raia kudhuru na kutwaa uhai wa wenzao.
"Chadema kama muumini wa haki za binadamu inayojumuisha haki kuu ya kuishi, inasikitishwa na machafuko haya yanayoondoa haki ya usalama na sio tu kwa wageni hata kwa wenyeji," imesema.
Taarifa hiyo imewasihi raia wa Afrika Kusini kuwachukulia waafrika wenzao kutoka mataifa mengine kama ndugu zao ambao kwa pamoja walishirikiana kupambana na ubaguzi wa rangi na hatimaye kuleta uhuru kwa taifa hilo.
"Ni muhimu mkatatua matatizo yenu ya ndani hasa ya kiuchumi kwa kushirikiana na wenzao wa mataifa ya Afrika waishio nchini humo na sio kuwaona kama maadui zao," ilisema.
Pia taarifa hiyo imesema kuwa ni muhimu serikali za Afrika kujikita katika kupambana na umasikini kwa kutengeneza fursa za ajira kwa raia wake ili kupunguza hasira za watu wao.
"Jumuiya za kikanda na Umoja wa Afrika wenyewe (AU) ni muhimu zikaweka msisitizo wa ukombozi wa kiuchumi unaoweza kukidhi haja na matakwa ya raia wa bara hili," imesema.
Chadema kimesema kuwa kuna madai kuwa hadi sasa raia wa Tanzania wawili wameuwawa katika ghasia hizo.
"Serikali ya Tanzania inapaswa kuyachukulia haya yanayoendelea kama tahadhari kwani hali ya umasikini na ukosefu wa ajira hapa nchini ni kubwa kiasi cha kuibuka kwa vikundi vya kihalifu vya komando Yoso na Panya Road vilivyofanya mashambulizi na uporaji kwa raia wengine," imeleleza.