Sunday, April 19, 2015

UCHUNGUZI KUHUSU MTOTO ANAYEDAIWA KUFUFUKA UMEFIKIA HATUA NZURI-POLISI


UCHUNGUZI KUHUSU MTOTO ANAYEDAIWA KUFUFUKA UMEFIKIA HATUA NZURI-POLISI
Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni, limesema kuwa uchunguzi wa maajabu ya kufufuka kwa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ( jina linahifadhiwa), umefikia sehemu nzuri na wakati wowote  matokeo yatakabidhiwa kwa Mwanasheria wa Serikali kwa hatua zaidi.



Mtoto huyo anadaiwa kufariki dunia mwezi Agosti, mwaka jana, baada ya kuugua ghafla na kuzikwa makaburi ya Mloganzila, Kibamba nje kidogo ya  jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa mtoto huyo alifufuliwa na Juma Nakochinya (33) maarufu kama Bino, mkazi wa eneo la Pandambili, mkoani Dodoma.

Mtoto huyo anadaiwa kuishi kwa Bino miezi kadhaa, ambapo Ijumaa iliyopita alipelekwa Dar es Salaam kwa wazazi wake kusalimia na kusababisha mamia ya wakazi kufurika nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo kushuhudia maajabu hayo.

Wazazi wa mtoto huyo, Hellena Mtoro (23) na baba yake Emmanuel Joseph  (32) na Bino, walilazimika kwenda polisi kutoa taarifa na uchunguzi ulianza kufanyika.

Kamanda Msaidizi wa mkoa huo wa kipolisi (ACP), Emmanuel Nley, aliliambia NIPASHE Jumapili juzi kuwa, uchunguzi wa tukio hilo umefikia hatua za mwisho.

Nley alisema kwa mujibu wa sheria, uchunguzi unapokamilika jalada la kesi kupelekwa kwa mwanasheria wa serikali ambaye ana uwezo wa kuifikisha mahakamani au la.

Alisema mwanzoni mwa wiki hii mtoto huyo alipelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi. Alisema  wanachosubiri ni majibu ya kitaalam kutoka kwa daktari.

Kuhusu kufukua kaburi ili kujiridhisha kama mtoto huyo alizikwa, Kamanda Nley alisema kuwa, ikiwa kutakuwa na kesi, amri hiyo hutolewa na mahakama.
Baba wa mtoto huyo Joseph alisema kuwa, mtoto wake amerudi juzi Dodoma kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.

Aliongeza kuwa, baada ya kukaa nyumbani hapo kwa muda wa siku mbili wananchi walianza kumzoea na kumuona mtu wa kawaida.

Alisema Bino ambaye ndiye aliyewasaidia kumpata mtoto wao, yupo jijini Dar es Salaam akiendelea kuwahudumia watu wengine wanaotaka huduma zake.

NIPASHE ilipowasiliana na Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Cyprian Mpemba, Alhamisi ya wiki hii ili kujiridhisha kama mtoto huyo alikufa kwenye hospitali ya Tumbi kama wazazi wa moto walivyodai, aliahidi kuifanyia kazi.
Jana alipopigiwa kuulizwa mkurugenzi huyo alimjibu mwandishi kuwa alikuwa kwenye mahafali.