WANANCHI mkoani Dodoma wamekuwa na maoni tofauti kuhusu hatua ya Jeshi la Polisi nchini, kuweka chini ya ulinzi vituo vitatu vya kulelea watoto vilivyokuwa vikifundisha dini ya Kiislamu na kareti.
Wengi wa waliohojiwa, walisema kuwa wanakerwa na hatua ya vituo hivyo, kuchanganya masomo ya dini na mchezo huo wa kareti na walitaka mamlaka husika, zikomeshe jambo hilo.
Mkazi wa Kikuyu, Bahati Bolibo alisema kuna haja ya Serikali kuhakiki upya vituo vya kulelea watoto, kwani vingi vinaendeshwa kinyume cha sheria.
Alisema vituo vingi vimekuwa vikianzishwa, lakini hakuna ufuatiliaji wa moja kwa moja unaofanyika ili kufahamu vimeanzishwa kwa lengo gani. "Jambo la msingi ni kuhakiki vituo vyote ili vijulikane na shughuli zake zijulikane zinaendeshwaje… kusajili tu kituo haitoshi," alisema Bolibo.
Kwa upande wake, akizungumza na gazeti hili, Mratibu wa Taasisi ya Kiislam ya Dalai Islamic Centre, Rashid Bura alisema Serikali inatakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili kufahamu kama vituo vya madrasa vinatumika kwa malengo tofauti.
"Madrasa yalikuwepo tangu enzi za mitume na watu wasitumie utashi wao kuonesha kuwa yanatumika kinyume na utaratibu… hizo ni propaganda tu kusikia kuwa madrasa yanatumika kufundisha kareti kwa vijana na watoto," alisema.
Alisema ni vyema uchunguzi wa Polisi, ubainishe ukweli ni upi ili kutoingilia uhuru wa watu wengine kuabudu. "Si dhambi kumtoa mtoto mkoa moja kwenda mkoa mwingine kwa ajili ya kumsomea dini," alisema Bura.
Jeshi la Polisi lililazimika kuweka chini ya ulinzi vituo hivyo, vilivyokuwa na watu 115 wakiwemo watoto. Majirani wa vituo hivyo, walidai kuwa watoto hao walikuwa wakipatiwa mafundisho ya dini ya Kiislam na kareti na wametoka katika mikoa 14 nchini, huku asilimia kubwa ya watoto hao wakitoka katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema bado Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wake, utakaohusisha kuhoji wahusika. "Wanaohojiwa ni wengi lakini bado idadi kamili sina ila ni wengi," alisema.