Kilombero. Wakati              msikiti wa Sunni uliopo Kidatu wilayani Kilombero ukimkana              Hamadi Makwendo aliiyeuawa katika tukio la kuwakamata watu              10 wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi, dereva wa              bajaji iliyowabeba baadhi ya watuhumiwa hao, amemuelezea mtu              huyo kuwa alikuwa hana shughuli za kikazi zaidi ya kucheza              karate.
          Polisi aliyejeruhiwa              kwenye sakata hilo na ambaye amehamishiwa kwenye hospitali              ya polisi mjini Morogoro, pia amesimulia mkasa uliosababisha              ajeruhiwe huku kukiwa na taarifa kuwa watuhumiwa hao 10              wamehamishiwa jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.
        Watu hao walimakatwa              mapema juzi usiku kwenye msikiti wa Sunni uliopo Kidatu              baada ya wasamaria wema kulitaarifu Jeshi la Polisi kuhusu              kuwapo kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu. 
        Habari za uhakika              zilizopatikana ndani ya Jeshi la Polisi zinasema watuhumiwa              hao wamehamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya              mahojiano zaidi.
        Kamanda wa polisi wa              mkoani hapa, Leonard Paul (pichani) hakupatikana kuzungumzia              suala hilo na hata alipotafutwa kwa simu, mlinzi wake              alipokea na kueleza kuwa bosi huyo wa polisi alikuwa kwenye              kikao kuanzia asubuhi na hakujua angemaliza wakati gani.
        Mmoja wa viongozi wa              msikiti wa Masjid Salah Al – Fajih, Mohamed Manze alisema              wao kama viongozi na waumini hawakuwa na taarifa zozote za              ujio wa watuhumiwa hao, na kwamba katika msikiti huo wapo              vijana wanne ambao huwa wanalala na kujisomea.
        Alisema siku ya  tukio              watuhumiwa hao walifika msikitini hapo saa 4:00 usiku wakati              ibada ya mwisho ikiwa imeshafanyika na waumini kutawanyika.
        Alisema walitumia mwanya              huo kuingia na kujihifadhi bila taarifa zozote kwa uongozi              wa msikiti huo, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu za              msikiti.
        Hata hivyo, kiongozi huo              alisema hawakupendezwa na suala hilo na kwamba limewachafua              na kuwaharibia sifa waumini na msikiti wao. Alisema mtu              aliyeuawa hakuwa muumini wa msikiti huo na hafahamiki.
        Alisema hawana nasaba na              kikundi chochote kinachojihusisha na uhalifu, na kulaani              vikali watu wanaotumia dini hiyo katika masuala aliyoyaita              kuwa ya kihalifu.
        Dereva wa bajaji asimulia
        Dereva  wa bajaji              iliyobeba watuhumiwa hao katika kijiji cha Kidatu wilayani              Kilombero, Alphonce Maulusi amemwelezea Hamad Makwendo,              aliyeuawa kwenye tukio hilo kuwa  ni mtu aliyekuwa              akijihusisha na mchezo wa kareti  pamoja na masuala ya dini              na hakuwa na kazi maalumu
          Mulusi alisema hayo                jana wakati akiongea na waandishi wa habari waliotembelea                kijijini hapo kwa lengo la kupata  undani wa tukio                lililotokea juzi katika kijiji cha  Chikago kata ya Kidatu                wilayani Kilombero ambapo watu 11 walikamatwa na polisi                 msikitini wakiwa na vifaa mbalimbali vya milipuko pamoja                na sare za jeshi.
          Alisema siku ya tukio                 majira ya saa 3:00 usiku akiwa katika eneo lake la kazi,                walitokea watu 11 na kwamba watano kati yao pamoja na                mwenyeji ambaye ni marehemu walipanda katika bajaji yake ,                na wengine sita walipanda katika bajaji ya mwenzake.
          Alisema watu hao                wakiongozwa na mwenyeji wao walitaka wapelekwe msikiti wa                Sunni na kwamba wakati wote wa safari yao mwenyeji wao                ndiye alikuwa akizungumza lugha ya Kiswahili huku wenzake                wakisikiliza bila kujibu.
          "Tuliwafikisha hadi                eneo walilotaka na kisha tuligeuza na yule mwenyeji wao.                Tulipofika Manyasini, tulisimamishwa na polisi waliotaka                kujua tumetoka wapi na tunaenda wapi. Yule mwenyeji                alishuka na kuanza kukimbia jambo lililofanya askari                kuanza kumkimbiza huku sisi tukifuatilia nyuma," alisema.
          Alisema mwenyeji huyo                alipofika mbele kidogo alimkata polisi mmoja na jambia  na                ndipo polisi walimpiga risasi na baadaye kumchukua na                kumpandisha katika gari lao.
          Alisema wananchi                walifika katika eneo hilo na kuzingira gari hilo na                kumshusha mtu huyo, huku wakitishia kuchoma moto gari la                polisi . Akizungumzia  mwonekano wa watu hao, dereva huyo                alisema walivalia mavazi ya jamii ya kabila la Wahindi                maarufu kama Panjabi na umri wao ukionekana kati ya miaka                20 hadi 25 tofauti na mwenyeji wao aliyeonekana mkubwa wa                zaidi ya miaka 30.
          Koplo Nasoro Dabi,                ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo, alisema siku ya                tukio, akiwa na askari wenzake walisimamisha bajaji                iliokuwa na abiria mmoja,  Hamad Makwenda.
          Alisema baada ya                bajaji hiyo kusimama marehemu alikimbia hali, iliyoashiria                kuwa ni mhalifu na hivyo kuwalazimu askari watatu, akiwamo                yeye, kumkimbiza.
          "Wakati tukimkimbiza,                mimi nilikuwa mbele na tulipofika katika eneo lenye giza,                alichomoa jambia na kuanza kunishambulia. Askari wenzangu                waliokuwa nyuma yangu walifyatua risasi na kupiga nyingine                juu hali iliyosababisha wananchi wengi kujitokeza na                kuanza kumpiga kisha kumchoma moto," alisema.
          Alisema wakati tukio                hilo likiendelea askari wengine walifanya mawasiliano na                mkuu wa  kituo cha Ruhembe na kuwaongezea nguvu.
          Mwenyekiti wa kitongoji
          Mweyekiti wa kitongoji                cha Ikera, Mohamed Libaha alisema siku ya tukio hilo                alifuatwa na askari saa 8:00 usiku na kutakiwa atoe malezo                kama ana taarifa za wageni katika kitongoji chao.
            Alisema bada ya kuwaambia kuwa                  hawana ugeni wowote, polisi waliwachukua watu hao pamoja                  na kiongozi wao wa dini, Ustadhi Maulid Sultani na                  kuondoka naye na hadi sasa hawana taarifa ya mintaarafu                  ya kiongozi huyo.
            MWANANCHI