Friday, February 06, 2015

Walimu wanaokaimu Utendaji kata kukiona



Walimu wanaokaimu Utendaji kata kukiona
OFISI ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeagiza kupewa majina ya walimu watakaobainika kukaimu nafasi za maofisa utendaji kata ifanyie kazi suala hilo.

Naibu Waziri, Aggrey Mwanri aliliambia Bunge jana kwamba hakuna mwalimu anayeruhusiwa kutoka kwenye kazi yake ya kufundisha na kwenda kukaimu ofisi hiyo.

Badala yake, alisema wanaotumiwa kwa ajili ya kukaimu Ofisi ya Mtendaji wa kijiji na kata, ni waratibu elimu kata na si vinginevyo.
"Kama tuna walimu waliotoka madarasani kwenda kukaimu, tupeni majina. Anayezungumziwa hapa ni mratibu elimu kata," alisema Mwanri akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko (Chadema) aliyehoji sababu za kutumia walimu kukaimu katika ofisi hizo.

Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Rosweeta Faustin (CCM) alisema baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Rukwa zina maofisa watendaji wa vijiji na kata ambao wengi wao hawajaariwa isipokuwa wanakaimu nafasi hizo kwa kipindi kirefu cha kati ya miaka mitatu hadi mine.

Naibu Waziri alikiri kuwapo baadhi ya vijiji na kata katika halmashauri ya Kalambo vyenye watendaji wanaokaimu. 
  
Alisema azma ya Serikali ni kuhakikisha nafasi wazi zinajazwa na kuondokana na watendaji kukaimu kwa muda mrefu.