Friday, February 06, 2015

Mzizi wa fitna kwa madiwani wa CHADEMA Waliofukuzwa Jijini Mwanza Kukatwa


Mzizi wa fitna kwa madiwani wa CHADEMA Waliofukuzwa Jijini Mwanza Kukatwa

JOPO la wanasheria lililoundwa kutoa tafsiri ya sheria katika sakata la kufukuzwa kwa madiwani watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Halmashauri ya Ilemela, mkoani Mwanza, limekamilisha kazi yake.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema jana bungeni kwamba juzi alisaini barua kwenda Tamisemi akitoa uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo.
Pinda alisema hayo wakati akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (Chadema) aliyesema ni miaka miwili imepita, lakini amekuwa hapatiwi majibu yenye matumaini juu ya suala hilo.
Katika sakata hilo ambalo madiwani walifukuzwa kwa kutohudhuria vikao vitatu vya kawaida vya Baraza la Madiwani, Kiwia alitaka kufahamu mustakabali wa kata za Kirumba, Nyamanoro na Ilemela mbazo zimekosa uwakilishi kutokana na hatua hiyo ya kufukuzwa.
Pinda alisema tatizo limekuwa la kisheria zaidi kuliko walivyofikiria."Tuliunda jopo kutoa tafsiri ya sheria na tumemaliza kazi. Juzi nilisaini barua kwenda Tamisemi nikitoa uamuzi wa mwisho," alisema.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge Kiwia aliyeomba wananchi wa kata husika wahakikishiwe ni lini uamuzi utawafikia, Pinda alisema, alisaini uamuzi huo akiwa Dar es Salaam na kuupeleka kwa Waziri wa Tamisemi.
Alisema anaamini taarifa haitachukua muda mrefu kutolewa Tamisemi kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.