Na John Gagarini, Kibaha.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi Nchini (NEC) imesema kuwa itahakikisha kuwa inaweka miundombinu mizuri kwa watu wenye ulemavu wakati wa uboreshaji wa zoezi la Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakalofanyika hivi karibuni.
Kutokana na umuhimu wa zoezi hilo Tume imejipanga kuhakikisha kila kundi ndani ya jamii ikiwemo ile ya walemavu wanashiriki kikamilifu zoezi hilo ambalo litaambatana na utoaji wa vitambulisho vipya vya wapiga kura vitakavyotumika kwenye wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na makamu mwenyekiti wa (NEC) Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, wakati wa mkutano wa Tume na waandishi wa habari wa mkoa wa Pwani juu ya uboreshaji wa Daftari hilo la wa Wapiga Kura. "Tumejipanga kuhakikisha hata watu wenye ulemavu wakiwemo, wasioona, walemavu wa viungo, viziwi na ulemavu wa aina yoyote ile kwani nao wanahaki ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka," alisema Jaji Hamid.
Aidha alisema kuwa kwa wale wasio na viungo vya mikono (vidole) watatambulika kwa sura kupitia picha lakini kwa wale wasio na tatizo watachukuliwa alama za vidole 10 vya mikono, sahihi na picha. "Zoezi hilo litatumia teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR) ambayo itachukua taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika kanzi data (Database) kw ajili ya utambuzi ambapo mfumo huu utasaidia kuwa na daftari sahihi na linaloaminika zaidi kwa ajili ya upigaji kura za maoni na uchaguzi mkuu wa 2015," alisema Jaji Hamid.
Jaji Hamid alisema kuwa kwa zoezi hilo vituo vitasogezwa na kuwa vingi zaidi ili kurahisisha walengwa kupata huduma karibu zaidi badala ya kutembea umbali mrefu. Kwa upande wake mkurugenzi wa sera na mipango wa NEC Orgenia Mpanduji alisema kuwa waandishi ni kiungo muhimu cha kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi hilo ambalo litakuwa la siku 14.
Mpanduji alisema kuwa endapo wananchi watshindwa kutumia kipindi hicho kuboresha taarifa zao watakuwa hawawezi kupiga kura hivyo ni vema wakatumia fursa hiyo ili kufanikisha zoezi hilo litakalowapatia vitambulisho ambavyo vitatumika kwenye zoezi la upigaji kura tu pekee.