Na Hassan Hamad (OMKR). Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF Taifa wamepitisha mapendekezo mbali mbali yaliyowasilishwa na Baraza Kuu la uongozi la chama hicho kuhusu marekebisho ya baadhi ya vipengele vya katiba ya chama hicho. Katika mkutano mkuu wa chama hicho unaoendelea kwa siku ya tatu katika ukumbi wa Ubungo Plaza Dar es Salaam, wajumbe hao pamoja na mambo mengine wamekubaliana kuwa mkutano mkuu wa chama hicho ufanyike mara moja katika kipindi cha miaka mitano badala ya miaka miwili na nusu kama ilivyopitishwa na mkutano mkuu mwaka 2009.
Katibu Mkuu wa chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuona kuwa mapendekezo yaliyopitishwa mwaka 2009 hayatekelezeki kutokana na ukosefu wa fedha unaokikabili chama hicho.
Hata hivyo amesema kwa mujibu wa sheria hiyo mkutano mkuu taifa unaweza kufanyika kwa dharura wakati wowote utakapohitajika. Wajumbe wa mkutano huo pia wamekubali mapendekezo ya kuongezwa ngazi ya uongozi ya Jimbo kwa upande wa Tanzania Bara ambapo kabla ya hapo hawakuwa na ngazi hiyo. Mapendekezo mengine yaliyopitishwa ni kwa Mwenyekiti wa chama hicho kupewa uwezo wa kuongeza wigo wa uteuzi kwa wajumbe wa kamati tendaji taifa, nje ya wajumbe wa baraza kuu na mkutano mkuu kwa kadri anavyoona inafaa kwa maslahi ya chama.
Aidha wajumbe hao wamekubaliana kuwepo kamati ya nidhamu na maadili kikatiba katika ngazi zote za uongozi kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa, sambamba na mambo ya uchaguzi kuondolea kwenye katiba na badala yake yabakie kwenye kanuni.
Kwa upande mwengine wajumbe wa mkutano huo wamekataa pendekezo la kuwepo uongozi katika ngazi ya Mkoa kwa upande wa Tanzania Bara, na kutaka ngazi za uongozi ziendelee kama kawaida kwa kuwepo ngazi ya Wilaya ikifuatiwa na ngazi ya Taifa.
Wajumbe hao wamekataa pendekezo hilo kwa madai kuwa ngazi hiyo itaongeza utitiri wa viongozi wasiokuwa na ulazima kwa maendeleo ya chama.
Pendekezo jengine walilolikataa ni uteuzi wa makatibu wa Wilaya ambapo wamekubaliana kuwa makatibu wa ngazi hiyo waendelee kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Wilaya. Marekebisho ya katiba hiyo yakayoingizwa kwenye "Katiba ya CUF ya mwaka 1992 toleo la 2014", yataanza kutumika kuanzia tarehe 22/08/2014.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiunga mkono moja ya hoja za marekebisho ya katiba ya CUF yaliyofanywa katika ukumbi la Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akiunga mkono moja ya hoja za marekebisho ya katiba ya CUF yaliyofanywa katika ukumbi la Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF Taifa wakiunga mkono moja ya hoja za marekebisho ya katiba ya CUF yaliyofanywa katika ukumbi la Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF Taifa wakiunga mkono moja ya hoja za marekebisho ya katiba ya CUF yaliyofanywa katika ukumbi la Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akitoa ufafanuzi juu ya hoja ya marekebisho ya katiba ya CUF yaliyofanywa katika ukumbi la Ubungo Plaza Dar es Salaam. (Picha na Salmin Said, OMKR)