Friday, February 06, 2015

Kamati ya Bunge Yataka walimu Wote Nchini Wasajiliwe



Kamati ya Bunge Yataka walimu Wote Nchini Wasajiliwe

KAMATI ya Bunge ya Huduma za Jamii imetaka walimu nchini kusajiliwa ikiwa ni pamoja na wanaofanya kazi katika shule binafsi ili kuwatambua na kuweka kiwango cha msingi cha kutoa huduma kote nchini.
Kamati hiyo ilisema kazi hiyo ifanywe na Tume ya Utumishi wa Walimu inayotarajia kuanza katika mwaka wa fedha 2015/16. Aidha, kamati hiyo imesema ili kukabiliana na changamoto ya Serikali kudaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) zaidi ya Sh bilioni 93.3 mpaka mwisho mwa mwaka jana, ikataka Bunge kutunga sheria maalumu itakayoweka utaratibu wa fedha za MSD kupelekwa moja kwa moja kama ilivyo kwa ujenzi wa barabara.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Margaret Sitta alisema kamati inapongeza kusudio la Serikali kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu nchini katika mwaka wa fedha 2015/16.
Alisema kamati inashauri tume hiyo kuanzishwa haraka ili kukabiliana na adha zinazowakabili walimu nchini na kurejesha hadhi ya taaluma ya ualimu nchini. Akizungumzia deni la Serikali kwa MSD, alisema deni hilo la bilioni 93.3 linachangia kwa kiasi kikubwa upungufu wa dawa vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini.
Sitta alisema pia kiwango cha Bajeti ya Sekta ya Afya kilichopendekezwa na Azimio la Abuja la mwaka 2001 kizingatiwe.