Thursday, August 20, 2015

Fukwe nadhifu Mtwara zinavyovuta watalii



Fukwe nadhifu Mtwara zinavyovuta watalii
Suleiman Msuya
MFUMO wa utawala wa kikoloni uliigawa Tanzania katika majimbo manane. Mkoa wa Mtwara ulikuwa ndani ya Jimbo la Kusini ambalo lilijumuisha mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara ambapo makao yake makuu yalikuwa Lindi.
Mkoa wa Mtwara ulipoanzishwa ulikuwa na wilaya tatu ambazo ni Masasi iliyoanzishwa mwaka 1928 chini ya Koloni la Kijerumani, Newala mwaka 1956 chini ya Koloni la Kiingereza na Mtwara ilianzishwa mwaka 1961.
Kutokana na ongezeko la watu na kukua kwa Mkoa wa Mtwara, ziliongezeka wilaya nyingine mbili ambazo ni Tandahimba iliyoanzishwa mwaka 1995, kutoka kwenye Wilaya ya Newala, na Nanyumbu ilianzishwa mwaka 2006 kutoka Masasi. Kiutawala mkoa huo umegawanyika katika wilaya 5 na halmashauri 9.
Mtwara ni kati ya mikoa 30 ya Tanzania. Uko katika upande wa Kusini-Mashariki mwa Tanzania. Umepakana na Mkoa wa Lindi upande wa Kaskazini, Bahari Hindi Mashariki, Msumbiji Kusini na Mkoa wa Ruvuma upande wa Magharibi.
Mkoa wa Lindi umepakana na mikoa ya Pwani, Mtwara, Ruvuma na Morogoro. Upande wa mashariki hupakana na Bahari Hindi. Mkoa huu umeanzishwa mwaka 1971 una eneo la kilimita za mraba 67,000. Karibu robo ya eneo lake au 18,000 ni sehemu ya hifadhi ya wanyama ya Selous.
Mkoa una wilaya sita za Lindi Mjini na Lindi Vijijini, Kilwa, Nachingwea, Liwale na Ruangwa.
Mito mikubwa ni Lukuledi, Matandu na Mavuji, yote inaelekeza maji yake katika Bahari Hindi. Mwinuko huanza mwambao ukipanda hadi mita 500, hauna milima mirefu.
Pamoja na historia ya muda mrefu ya mikoa hiyo kiuhalisia inaonekana bado ipo nyuma kiuchumi huku sababu ikielezwa kuwa ni kuwa ilisahauliwa.
Hali ya kuwa nyuma kwa miaka mingi inaanza kuondoka katika mikoa hiyo ambayo imeanza kugundua fursa mbalimbali za kiuchumi katika kuendeleza huduma za kijamii kama gesi, mafuta na nyingine nyingi.
Awali mikoa hiyo ilitambulika kwa kuzalisha zao la korosho ambapo kimsingi bila kupepesa macho zao hilo halijawa na tija kwa jamii ya mikoa hiyo hali ambayo ilisababisha uendelee kuwa nyuma kimaendeleo.
Katika jitihada za kuhakikisha kuwa mikoa hiyo inafunguka kiuchumi Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuongeza nguvu ya kuboresha miundombinu hasa ya barabara na madaraja ili kufungua fursa zilizopo.
Serikali ya awamu ya tatu pamoja na ya nne zilijikita katika kuboresha miundombinu hiyo ili iwe kichocheo cha kukuza uchumi katika mikoa hiyo jambo ambalo limeonekana dhahiri kuwa mabadiliko yatapatikana kwa wakati na haraka.
Jamii ya mikoa hiyo imekuwa ikijitahidi kubuni fursa ambazo zinaendana na uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi ambapo kila kukucha wanaongezeka.
Inasemekana kuwa zaidi ya wawekezaji 56 wanatarajiwa kuwekeza katika kipindi kifupi kwenye mikoa hiyo huku hitaji kuu likiwa ni kupatikana kwa ardhi, maji na umeme wa kutosha wa kuhudumia uwekezaji wao.
Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha au kuwaasa wananchi wa mikoa pamoja na Serikali kutumia kila mbinu ambayo inaweza kuwapatia wawekezaji hao ardhi ili kukuza uchumi wa mikoa hiyo ambayo ilibakia nyuma.
Hakuna shaka kuwa mikoa hiyo ilibakia nyuma baada ya miundombini kutokuwepo hilo limemalizwa na Rais Jakaya Kikwete kupitia Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli ambaye amehakikisha kuwa mikoa hiyo inafunguka.
Iwapo hilo la barabara limewezekana nadhani wakati wa kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha wawekezaji wanapatiwa ardhi ili waje kuwekeza ni jambo muhimu kwa kila mdau.
Nakumbuka Rais Kikwete akiwa katika ziara ya kuwaaga wakazi wa mikoa hiyo aliweka bayana kuwa uchumi wa mikoa ya kusini hakuna wa kuuzuia kwani ni jambo la lazima.
Kama hivyo ndivyo naaamini wataka urais wajao wanapaswa kutambua kuwa kusini ndiyo mashine ya kuendesha uchumi wa Tanzania kwa miaka ijayo hivyo ni wajibu waelekeze nguvu zao katika maeneo hayo hasa katika kufanikisha ardhi inapatikana, umeme wa uhakiki na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Tumeshughudia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeamua kufungua ofisi ya kanda katika Mkoa wa Mtwara, ujenzi wa hospitali ya rufaa katika mikoa hiyo vyote hivyo ni juhudi ambazo wataka urais wanapaswa kuziendeleza ili kuendeleza mikoa hiyo.
Kampuni ya kuzalisha Saruji ya Dangote ili izalishe mbolea inatajwa kuwa zitatoa ajira zaidi ya 15,000 kwa Watanzania wengi hivyo kinachohitajika ni kuhakikisha kuwa ardhi inayohitajika inapatikana kwa wakati ili kuhakikisha kuwa uchumi na maendeleo ya mikoa hiyo inapaa.
Mtwara na Lindi wamejitahidi pia katika kasi ya kujenga nyumba za kufikia wageni mbalimbali ambao wanaotembelea mikoa hiyo pamoja na ukweli kuwa hitaji bado ni kubwa hasa pale panapokuwa na matukio mbalimbali ya kitaifa.
Hivi karibu kulikuwa na sherehe za nane zilizofanyika katika Mkoa wa Lindi, wageni walikosa nafasi za kulala hivyo kulazimika kwenda mkoani Mtwara ambapo ni kilometa 95 kutoka Lindi Mjini.
Kasi ya ujenzi pia inapaswa kuzingatia ubora kwani hakuna shaka kuwa mikoa hiyo inaendelea kukua kiuchumi hasa kwa gesi ambayo inapatikana kwenye maeneo hayo.
Pamoja na yote ambayo nimeyaelezea awali ya kuitaka Serikali inapaswa kuwekeza nguvu kubwa hasa kuhakikisha kuwa kila sekta inakwenda pamoja na maendeleo ambayo yanapatikana yana akisi jamii yote.
Aidha, napenda kutumia nafasi hii kupongeza mikoa ya Kusini kwa kutunza Ukanda wa Bahari ya Hindi jambo ambalo linashawishi mtu kutamani kutembelea mwambao wa bahari hiyo kwa kuvutiwa na usafi uliopo.
Katika hili huhitaji kuhadithiwa kwani ni dhahiri kuwa Mtwara maji yake ya bahari ni masafi aidha pembezoni mwa bahari hakuna uchafu kama kulivyo katika ukanda huo kwa eneo la Mkoa wa Dar es Salaam.
Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam mnapaswa kwenda kujifunza Mtwara hasa katika utunzaji wa mazingira katika maeneo ya mwambao wa bahari.
Nakumbuka kauli ambazo walizitumia wabunge wa Mtwara na Lindi katika maonesho ya nanenane kwa kumuita Rais Kikwete shemeji unatuachaje naamini wanajua ameawaachaje hivyo vilivyobakia ni wajibu wao kutengeneza mazingira rafiki ili waweze kufikia malengo yao.
Nimependa kutumia ukurasa huu kuwakumbusha wana Mtwara kuwa fursa zilizopo sasa wakizitumia ipasavyo watakuwa na mafanikio chanya ambayo hayatasahaulika kama wanavyoshindwa kusahau kuhusu wao kubakia nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi.