Sunday, July 12, 2015

Mkapa, Mwinyi na Karume wainusuru NEC


Mkapa, Mwinyi na Karume wainusuru NEC
Kutoka kushoto ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi,Rais mstaafu wa  awamu ya tatu Benjamin  Mkapa na wa mwisho kulia ni Rais Mstaafu wa Zanziba  Abeid Amani Karume na katikati ni Pius Msekwa.

Marais wastaafu watatu na makamu wa zamani wa CCM jana walifanya kazi kubwa ya kukinusuru chama hicho kuingia kwenye mgogoro uliokuwa unanukia baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais.
Kwa mara ya kwanza, wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya chama hicho juzi walijitokeza hadharani na kupinga uamuzi wa chombo hicho wa kupitisha majina ya wagombea kwa njia ambazo walisema zinazokiuka katiba ya CCM.
Kama hiyo haitoshi, jana wajumbe wa Halmashauri Kuu walimuweka mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kwenye hali ngumu baada ya kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani na Lowassa, likiwa ni tukio la kwanza la aina yake kwenye vikao vya juu vya chama na ambalo liliashiria kuanza kupoteza utii kwa chama.
Habari kutoka ndani ya NEC zinasema kuwa baada ya mapumziko ya chakula cha mchana, kikao hicho kilijadili kwa kirefu sakata la kuchujwa kwa Lowassa na pande zinazohusika zilizungumza kwa hisia kali, ndipo marais hao, Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Abeid Amani Karume na makamu mwenyekiti wa zamani, John Samuel Malecela walipolazimika kuingilia kati.
"Ilibidi kwanza wote waliokuwa wanagombea urais waondolewe kwenye mkutano ndipo tuanze kujadiliana," alisema mmoja wa wagombea ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mjumbe mwingine wa kikao hicho alisema Malecela, Mkapa, Karume na Mwinyi walitumia maneno ya busara na kuwatahadharisha wajumbe dhidi ya misimamo yao.
"Walituonya kuhusu kujali masuala yetu binafsi kuliko amani ya nchi na kututaka kuangalia sana misimamo yetu kwa kuwa inaweza kuhatarisha amani," alisema mjumbe huyo.
Alisema wakati kikao kilipositishwa kwa ajili ya chakula cha mchana, kuna baadhi ya wajumbe waliondoka eneo hilo na wengine kubaki, akiwamo Lowassa ambaye hakujulikana alielekea eneo gani kwenye jengo hilo.
Kikao cha mchana kilianza bila ya Lowassa kuwamo na Karume alianza kuzungumza, na kufuatiwa na Malecela, Mkapa, na Mwinyi, ambaye alipomaliza aliwashauri wajumbe kuwa waendelee na upigaji kura kwa kuwa suala hilo limeshaeleweka.
Mkutano ulipoanza kupiga kura ndipo Lowassa alipoingia na kukuta kazi ya upigaji kura inaendelea na hivyo kuendelea na shughuli hiyo.
Awali, kwa mara ya kwanza, Kikwete jana alikumbana na mapokezi ya aina yake wakati wajumbe walipomuonyesha waziwazi kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kwa kuimba wimbo wa kumuunga mkono Edward Lowassa kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu kuanza.
Hali hiyo imetokea wakati baadhi ya wanachama wa CCM wakiwa bado hawajakubali kuenguliwa kwa Lowassa kwenye kinyang'anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM baada ya Kamati Kuu kupitisha majina ya John Pombe Magufuli, Amina Salum Ali, Bernard Membe, January Makamba na Dk Asha Rose Migiro kwa ajili ya kupigiwa kura Halmashauri Kuu.
Hali ya kutoafikiana na uamuzi huo wa Kamati Kuu pia ilionekana nje ya jengo la makao makuu ya CCM, ambako kikundi cha watu ambao baadhi yao walivalia sare za CCM kiliimba jina la Lowassa wakati wajumbe wakiingia kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu.
Wakati Kikwete akiongoza viongozi wa juu kuingia kwenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kuendesha kikao cha Halmashauri Kuu, wajumbe walipaza sauti zao kuimba "tuna imani na Lowassa, oyaa, oyaa, oyaa. Lowassa kweli? kweli kweli kweli Lowassa...".
Rais Kikwete na viongozi wenzake walisita kuingia ukumbini, lakini baadaye aliingia katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akifuatiwa na Kikwete, makamu mwenyekiti wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na wa Bara, Phillip Mangula.
Wimbo huo uliongozwa na kundi lililokuwa nyuma ukumbini likijumuisha mfanyabiashara maarufu nchini, Christopher Gachuma, mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, aliyekuwa mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo na mjumbe mwingine aliyetambulika kwa jina la Joseph Marwa ambaye anatoka Mara. Wajumbe hao na baadhi wengine waliendelea kuimba wimbo huo kwa takriban dakika mbili kabla ya kunyamaza kumruhusu Kikwete afungue kikao.
"Kweli Haijawahi kutokea," alisema Rais Kikwete akionekana kusawajika. Na wajumbe walimjibu, "kweli". Akawauliza tena, "habari za asubuhi" na kujibiwa,"nzuri".
Kinana alisimama na kutangaza akidi kwamba idadi ya wajumbe inatakiwa kuwa 325 lakini waliohudhuria ni 274, sawa na asilimia 87, hivyo akidi imetimia.
Ndipo Kikwete alipoeleza ajenda za kikao hicho na jinsi kitakavyoendeshwa na akamaliza kwa kuwataka wajumbe wapunguze jazba.
"Matumaini yangu ni kwamba vikao vitakwenda vizuri, tutazungumza kwa utulivu. Tupunguze jazba. Unajua ukikasirika wakati mwingine hoja hazitoki sawasawa, kwa hiyo matumaini yangu makubwa ndiyo hayo. Ninawatakia kikao chema," alisema Rais Kikwete.
Afungua kikao
Akifungua kikao hicho, Rais Kikwete alisema mkutano huo una ajenda tatu.
"Karibu katika Mkutano wa Halmashauri Kuu Maalumu, kwa mujibu wa katiba yetu chama. Kikao hiki kitakuwa na ajenda; kupokea mapendekezo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020;  Kufuta kifungu cha kanuni kinachoweka ukomo wa ubunge na madiwani wa viti maalumu, mtakumbuka tulikuwa tumeweka ukomo wa vipindi viwili na sasa tunapoelekea kwenye mchakato wa Katiba Inayopendekezwa na haijapita, tumeona tufungue hiki kifungu ili itakapokuja Katiba mpya, basi tuwe tunafuata hayo ya Katiba Mpya yanayopendekezwa ya 50:50," alisema Kikwete.
Aliongea kuwa baada ya hapo itafuata ajenda ya kuchagua mwanachama anayependekezwa kugombea urais Zanzibar na mgombea urais wa Tanzania.
Baada ya kusema hayo, aliwataka waandishi wa habari kutoka ukumbini ili kikao kiendelee. Baadhi ya wajumbe walianza kuwasili kwenye eneo la jengo hilo wakiwa wamenuna na baadhi kupiga kelele kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ni chao hivyo wangeweza kubadilisha uamuzi wa Kamati Kuu.
Nje ya ofisi hizo za makao makuu ya chama hicho kulikuwa na mshikemshike baina ya wafuasi wa Lowassa na polisi.
Mapema asubuhi kabla ya wajumbe wa Halmashauri Kuu kuingia kwenye kikao, hali ilikuwa shwari na watu walikuwa kwenye makundi wakizungumzia matokeo ya mchujo wa wagombea urais.
Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walikuwa wamekaa ndani ya magari yasiyopungua matano kusimamia hali ya usalama wakati wajumbe wakiingia eneo hilo.
Barabara Kuu inayopita mbele ya jengo la makao makuu ya CCM ilifungwa kuanzia katika makutano na Barabara ya Mbeya karibu na ofisi za mkoa za Mamlaka ya Mapato (TRA) na mwanzoni mwa bustani ya Nyerere Square katika Barabara ya Lindi.
Kutokana na kufungwa barabara hiyo, foleni ndogo ilianza kwenye barabara za ndani iliyokuwa ikitengenezwa na magari ya wajumbe wa mkutano mkuu waliokuwa wakishuka eneo hilo kuchukua vifaa na daladala zilizokuwa zikifanya safari zake kati ya Jamatini na maeneo mengine ya mji.
Eneo lote linalozunguka ofisi za CCM zilijaa makada na wakazi waliokuwa wakipita kushuhudia wafuasi wa Lowassa waliokuwa wakipigania 'haki' ya kada huyo kubakizwa kwenye mchakato wa urais.
Saa 6:20 mchana, kikundi kidogo cha makada waliojiita wafuasi wa Lowassa kilianza kuimba "Lowassa, Lowassa. Tunamtaka Lowassa wetu".
Kikundi hicho kilizidi kukua na kuendelea kuimba kikiwa ndani ya uzio wa bustani ya Nyerere Square na kuvutia idadi kubwa ya watu na waandishi huku gari tatu za polisi zikiwa jirani kufuatilia mwenendo wao.
"Siku hizi tunakwenda na matakwa ya wananchi. Zama za kusema chama kwanza zimepitwa na wakati… lazima uwapatie wananchi mtu wanayemtaka. Huu siyo wakati wa chama kimoja ni wa vyama vingi ni lazima twende na nyakati na mahitaji ya sasa," aling'aka mtu aliyejitambulisha kwa jina la Michael William (65) aliyedai alijiunga na CCM tangu 1963.
Makada hao walienda mbali zaidi kudai uamuzi wa kumuengua Lowassa unaua chama hicho na kutishia kurejesha kadi za uanachama.
Baada ya nusu saa kundi hilo liliongezeka na kutoka nje ya uzio hadi karibu na Barabara ya Nyerere mkabala na ofisi za CCM ambako polisi walikuwa wamefunga barabara, na kutoa kashfa kwa viongozi wa chama hicho.
Pale waandamanaji walipojaribu kutaka kutawala eneo hilo, polisi walitumia magari yao kuwarudisha nyuma na kuwatawanya. Hata hivyo, liliendelea na harakati hizo kuimba bila kuchoka na kusababisha umati wa watu upande wa pili wa barabara.
Baadaye walianzisha vurugu na kusababisha mmoja wao kukamatwa na polisi kitendo kilichopunguza makali ya kundi hilo.
Wafuasi hao walikuwa wakiimba na kupaza sauti kuwa wapo tayari kupigwa mabomu kwa sababu ya Lowassa kuliko "kuendelea kuendekeza siasa za kubebana na kuwaacha watu wanaopendwa na wananchi".
Wakati makada hao wakiendelea na harakati hizo, hali ilikuwa mbaya kwa wauza nguo na bidhaa nyingine wa eneo hilo.
"Tulitegemea tungefanya vizuri kwenye biashara zetu leo lakini hao wafuasi wa Lowassa wanatuogopesha. Jana hali ilikuwa shwari lakini leo amani imetoweka na nahisi tutawahi kuondoka eneo hili licha ya ulinzi kuwepo kwa sababu haya maandamano yanaweza kuwa makubwa," alisema mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Maoja.
Awali mchana wakati wajumbe wakiingia kikao cha NEC, mjumbe wa Mkoa wa Simiyu, Dk Raphael Chegeni aliingia eneo la ofisi za Makao Makuu ya CCM huku akipaza sauti: "Hiki ni chama chetu, hiki ni chama chetu" akisema wanakwenda Halmashauri Kuu kuweka orodha ya wagombea wanaowataka na mmojawapo ni Edward Lowassa.
Mjumbe wa NEC, Wilaya ya Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi alisema Watanzania wategemee kwamba chombo hicho kitatenda haki na watapewa sifa za wagombea halafu wataamua.
"Tunashangaa Edward Lowassa hayumo kwa sababu tumeshuhudia jinsi anavyopendwa na ambavyo amekuwa akipokewa na wananchi," alisema Karamagi.
Zakia Meghji alisema siku zote wanafuata demokrasia, hivyo walianza na wagombea 41, juzi wamepatikana watano na hatimaye atapatikana mmoja.
Hata hivyo, alisema hajui iwapo inawezekana au haiwezekani NEC kuitisha majina ambayo yametupwa kama baadhi ya wenzake wanavyodai huku akishauri wasubiri waone.