Sunday, July 12, 2015

Waliokwama tano bora watema cheche



Waliokwama tano bora watema cheche
Aliyekuwa mgombea wa kuteuliwa na CCM kugombea kiti cha urais, Stephen Wasira akiwakimbia waandishi wa habari wasizidi kumuuliza maswali katika viwanja vya makao makuu ya chama hicho, mjini Dodoma jana.
 Aliyekuwa anawania kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho, Profesa Mark Mwandosya amesema atamuunga mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa.
Vilevile, Profesa Mwandosya amesisitiza kauli yake ya awali kuwa hatawania ubunge katika Jimbo la Rungwe Mashariki na tayari ameshawaaga wananchi wa jimbo lake.
Hata hivyo, Waziri huyo katika Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) alibainisha kuwa hawezi kustaafu siasa kwa sababu ni maisha ya kila siku kwa binadamu.
Akizungumza katika ofisi za Makao Makuu ya CCM mjini hapa jana, Profesa Mwandosya alisema: "Katika nyakati mbalimbali mataifa na binadamu hupita kwenye nyakati za majaribu, njia ambayo Mwenyezi Mungu huimarisha mtu na Taifa iwapo tutaweza kuyamudu. Hiki ndicho kipindi tunachopita sasa kama Taifa.
"Kwa maneno haya sasa napenda na kwa unyenyekevu mkubwa kuwashukuru kwa dhati kabisa wale wote mliotuunga mkono kabla na baada ya kutangaza nia, wakati na baada ya kuchukua fomu za kuomba nafasi hiyo kwa imani kwamba ninakidhi na pengine ninazidi vigezo vilivyowekwa."
Dk Kamani
Mgombea mwingine ambaye hakuchomoza katika tano bora, Dk Titus Kamani alisema hana mgombea anayemuunga mkono zaidi ya yule ambaye atasimamishwa na chama.
"Ninaviamini vikao vyetu vya chama, nafikiri wametumia muda wao vizuri, lakini kwa sababu vikao navyo vina ngazi mbalimbali. Kamati Kuu na zile za awali za maadili na sekretarieti zinaandaa uamuzi utakaoidhinishwa na Halmashauri Kuu, sasa ndiyo tunaingia, kwa hiyo tutaangalia watakachotuletea kama tutabariki au tutahitaji kuboresha," alisema na kuongeza.
"Maana ya mkutano lazima kuwe na mawazo tofauti, kama kusingekuwa na utofauti wa mawazo tungewaacha wakamalizia kulekule, lakini kwa sababu kuna tofauti ya ukubwa na mamlaka ndiyo maana NEC ipo."
Balozi Karume
Akizungumzia hatua hiyo, Balozi Ali Karume alisema hana tatizo na uamuzi wa CC. Alisema kwamba amesikia utaratibu utakuwa wa kupiga kura tatu kwenye NEC, hivyo kuahidi kwamba atashiriki kikamilifu kuhakikisha washindi wanapatikana.
"Simo katika watu wabishi, simo kwenye wanaouliza maswali, nasema CC imefanya kazi ngumu sana ikatuletea watu watano kumbukeni siyo mtu mmoja huyo, watano. Tutampata mmoja tunayemuamini kwamba anaweza akatuvusha kwenye hili.
"Simo katika utendaji nasikia maneno maneno mengi tu mitaani, sijui nchi nzima wameshafanya uamuzi kwamba wanampendelea bwana au bibi fulani, mimi hayo siyajui kwa sababu nchi yetu hii ni kubwa sana. Ukienda Zanzibar utaelezwa Karume nimemlea lakini tunazungumzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sitapenda wala kukubali kudanganywa kwamba kuna sehemu moja ya Tanzania wanampenda sana fulani basi tumpe huyo, mimi nasema hapana. Ninachoomba kwa chama changu ni kwamba tuepuke makundi haya, tumpate mtu ambaye kweli atakuja kuyafuta haya makundi halafu tuunde Serikali ambayo haina ubaguzi wa aina yoyote," alisema Balozi Karume.
Ngeleja
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alisema anaheshimu uamuzi huo kwa sababu CCM ina utaratibu wake na kila anayeingia anaufahamu, hivyo anaafiki utaratibu uliofuatwa ambao umekuwa ukifanyika miaka yote.
"Chama ndicho kinachoongoza taratibu kwenye michakato ya aina hii, tuliokuwa tunagombania nafasi moja na wote walioingia tulikuwa tunajinadi kuwa tunaweza, nafasi inakuwa ni moja na inapofikia hatua ya uamuzi tunasema kura hazitoshi lakini siyo kwamba waliobaki hawana uwezo wa kuongoza Taifa," alisema Ngeleja.
Chikawe
Mgombea mwingine ambaye hakupita katika mchujo wa awali, Mathias Chikawe alisema kumekuwa na kutokuridhika kwa baadhi ya wajumbe na wanachama wa CCM kutokana na jinsi uteuzi ulivyofanyika lakini kwa upande wake, alisema hana neno na uamuzi huo. Alisema kwa mtazamo wake, majina matano yaliyowasilishwa na Kamati Kuu yalichujwa na Kamati ya Maadili kinyume na ilivyotarajiwa akisema kamati hiyo ilipaswa kuwasilisha ripoti tu kuhusu watia nia. Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi alisema kutokana na wanaCCM kutokubaliana na uteuzi wa majina hayo huenda kukatokea mpasuko. Kuhusu jina lake kukatwa, Chikawe alisema hana na anaamini katika majina hayo matano ndipo atakapotoka kiongozi wa nchi aliyechaguliwa na chama.
Dk Mahiga Aliyekuwa Balozi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa (UN) Dk Augustine Mahiga alisema hana budi kukubaliana na uamuzi ya chama. "Huo ndiyo uamuzi wa chama, mimi nakubaliana nao ninaona wametenda haki tu."
Makongoro
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) na mtoto wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro alisema hajui ni wagombea gani waliopenya kwenye tano bora isipokuwa kusikia tetesi tu.
"Unajua mimi pia nasikia kuwa kuna majina yametoka, kwa bahati mbaya nimesikia tu kuwa Nape ameyataja lakini sijajua ni nani waliopitishwa," alisema.
Makongoro alisema pengine hao waliochaguliwa watafanya vizuri watakapopewa nafasi ya kuipeperusha bendera ya CCM."
Kuhusu jina lake kukatwa alisema hana kipingamizi kwani hiyo ndiyo demokrasia ya chama na lazima iheshimiwe.
Bilohe
Mmoja wa watia nia hao, Edelphonce Bilohe maarufu kama 'Mkulima' alilalamika na kusema kuwa hajaelewa mchakato mzima wa kuteua majina matano ulivyokwenda zaidi ya kushuhudia purukushani mjini Dodoma. Pamoja na kutoelewa mchakato wa uteuzi huo, Bilohe alilalamika kuwa tangu amefika Dodoma hajapata mapokezi mazuri kutoka kwa wana CCM wenzake au hata wale watia nia 38 waliobahatika kurudisha fomu. "Kila ninapojaribu kuuliza hiki au kile sipewi majibu, nimekaa hapa na wanaCCM wa mkoani, sijaonana na Nape (Nnauye) wala (Abdulrahman) Kinana, wala watia nia wenzangu," alisema.
Alisema anashangaa kuwa hajahojiwa kama utaratibu wa uteuzi huo unavyotakiwa badala yake ameshindwa hata kujua wanaCCM wenzake walipo na wanafanya nini kwa wakati huo.
"Kuna makundi hapa, hali si nzuri, mpaka sasa sijaelezwa utaratibu wa mkutano wa halmashauri unavyokwenda. Nimezunguka nchi nzima, nitawaambia nini Watanzania. Hali ya hapa imeharibika," alisema. Bilohe alisema hajaridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea na alieleza kufurahishwa kwake na hatua ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa kuyapinga.