Friday, February 06, 2015

Vocha bandia Shivacom, Voda zatikisa Bunge




Vocha bandia Shivacom, Voda zatikisa Bunge
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.

Wabunge wameishukia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushindwa kutunga kanuni za kutekeleza sheria ya mawasiliano na ya madini huku wakiibua sakata la vocha feki zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 500 ambazo serikali imeshindwa kukusanya kodi kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya kampuni ya simu ya Vodacom na Shivacom.
 
Wabunge hao waliibua suala la vocha feki wakati wakichangia taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kwa kipindi cha kuanzia Machi 2014 hadi Januari 2015.
 
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, akichangia hoja za kamati  juzi bungeni, alisema mwaka 2010 Bunge lilitunga sheria ya madini na sheria ya mawasiliano ambazo zilikuwa zikielekeza kampuni za simu na migodi ziorodheshwe kwenye masoko ya mitaji Tanzania kwa lengo la kuhakikisha hesabu zao zitakuwa wazi kusudi mapato na matumizi yaweze kufahamika  ili serikali itoze kodi sahihi.
 
Kafulila alisema ni aibu kwamba tangu mwaka 2010 Bunge lilipotunga sheria hizo kampuni za simu na migodi ya madini nchini zimeigomea na kuikatalia serikali kutunga kanuni na kusababisha sheria hiyo kushindwa kutekelezwa huku mawaziri wakiendelea kuwapo bungeni.
 
 "Miaka mitano Waziri wa Nishati na Madini ameshindwa kutengeneza kanuni za kuhakikisha migodi inaorodheshwa kwenye soko la mitaji ili tupate kodi sahihi, miaka mitano Wizara ya Mawasiliano, Sanyansi na Teknolojia imeshindwa kutengeneza kanuni kuhakikisha kampuni za simu ambazo zinavuna mamilioni ya fedha nchini kuorodheshwa kwenye soko la mitaji hii ni aibu,"alisema.
 
 Aliongeza kuwa kampuni mbili ambazo ni Vodacom na Shivacom zimekuwa katika mgogoro wa kutengeneza vocha 'feki' zenye thamani ya Dola za Marekeni milioni 350 sawa na Sh. bilioni 500.
 
 Alisema katika hali ya kushangaza serikali ilipoulizwa suala hilo ilisema huo ni mgogoro wa wafanyabiashara wawili, hivyo haihusiki bila kujua kwamba kuna suala la kodi ambazo serikali ilitakiwa kukusanya kutokana na vocha hizo.
 
 "Serikali inashindwa kuelewa katika suala hilo kuna kodi kwani katika vocha hizo kuna za Sh.500 na Sh.1,000 ambazo zinatumika na watu maskini sasa serikali hii dhaifu inashindwa kudhibiti kodi ya Sh. milioni 500," alisema.
 
Kafulila alisema inashangaza serikali kila siku inabaki kutegemea kodi kutoka kwa wafanyakazi na kusababisha Tanzania kuwa nchi ambayo inatoza kodi kubwa kuliko nchi zote za Afrika Mashariki kwa wafanyakazi.
 
"Tanzania inatoza kodi kwa wafanyakazi asilimia 18, Burundi asilimia 10.3, Uganda asilimia 11, Rwanda asilimia 6.9, wafanyakazi wanatozwa kodi kubwa kwa sababu migodi haitozwi kodi, mnaleta bajeti za njaa njaa hapa, nyie ni dhaifu kukusanya kodi kwa wenye fedha,"alisema.
 
Naye Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, alisema wanaisubiri serikali kutoa hesabu kuhusuiana na mgogoro kati ya Vodacom na Shivacom, kwa kuwa umesababisha serikali kukosa kodi.
 
Mpina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, alisema kumekuwa na mikataba yenye utata baina ya kampuni za simu kutokana na kukosekana kwa usimamizi thabiti na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato ya serikali na kuingiza hasara watumiaji wa simu. 
 
 Alitoa mfano wa kuvunjika kwa mkataba kati ya Shivacom na Vodacom Tanzania Limited (Contract for the Production of electronic recharge vouchers).
 
Alisema kamati yake inazo taarifa kwamba moja ya sababu ya mkataba wa Shivacom na Vodacom kuvunjika ni kutokana na Shivacom kuiibia Vodacom na wateja wake kwa kuzalisha vocha za kielektroniki na kuzisambaza moja kwa moja kwa wateja kwa kutumia namba za siri zilizotolewa na Vodacom na baadaye kuwasilisha vocha ileile kwa Vodacom Tanzania Limited ambazo hazina thamani.
 
 Alisema kutokana na mgogoro huo, Kamati imemuagiza Waziri wa Fedha kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia kuiagiza Mamlaka ya Udhibiti Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya uchunguzi dhidi ya madai hayo ili kubaini kiasi cha mapato ya Serikali yaliyopotea kutokana na mkanganyiko wa kampuni hizo.
 
  Mpina alisema kama itathibitika kuwa madai haya ni ya kweli basi Taifa litakuwa limepoteza mabilioni ya fedha kama kodi, wateja kukosa huduma na kuibiwa kwa kipindi chote cha kuanzia Julai, 2007 hadi Julai, 2012. 
 
 Aliongeza kuwa changamoto nyingine inayokwamisha mapato ya Serikali kwenye sekta ya mawasiliano ni uwapo wa sheria mbili tofauti za Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kunakosababisha usumbufu wa ukusanyaji wa kodi ya ongezeko la thamani. 
 
 Alisema kampuni za simu za Tanzania Bara yanayosababisha ankara katika kampuni za simu za Zanzibar (Zantel) malipo hufanywa bila Vat kwa madai kuwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar imekwisha kata kodi hiyo, na kwa upande wa Zanzibar wanapoleta ankara zao Tanzania Bara inakuwa hivyo hivyo. 
 
"Kamati inashauri Serikali ikutane na Mamlaka zote mbili ili kushughulikia tatizo hili la utata huu wa kodi,"alisema.
 
 Alisema kimsingi pamoja na watumiaji wa simu za mkononi kuongezeka, bado sekta ya mawasiliano haijachangia kikamilifu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.  Alitoa mfano kuwa mwaka wa fedha 2013/2014 mapato ya kodi yatokanayo na mawasiliano yalikuwa Sh. bilioni 576.46 tu.
 
Alisema mtambo wa Telecomunication Traffic Monitorig system (TTMS) ulitarajiwa kudhibiti mawasiliano ya ndani na nje, lakini cha kushangaza mtambo huo hivi sasa una dhibiti mawasiliano ya simu za nje pekee. 
 
 Mpina alisema TRA haijawa na uwezo wa kujua na kudhibiti mawasiliano ya simu (airtime traffic) yanayofanywa ndani ya nchi na hivyo ukokotoaji wa Vat na ushuru wa bidhaa (Excise duty) hutegemea takwimu na hesabu zinazotolewa na kampuni za simu husika.
 
Kuhusu ukusanyaji wa mapato kwenye sekta ya madini, alisema taarifa za Walaka wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Tanzania Extractive Industries Transparency Initiative (TEITI) zimekuwa zikiripoti upotevu mkubwa wa mapato katika biashara ya madini. 
 
Makampuni makubwa  ya madini yamekuwa yakikwepa kodi kwa kuongeza na kupunguza gharama za bidhaa na huduma huku madini mengi yakitoroshwa kupitia njia rasmi na zisizo rasmi.
 
 Alisema kamati inapendekeza Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ifanyiwe marekebisho ili kumuwezesha Kamishna wa Madini kutaifisha madini yanayopatikana kinyume cha Sheria na kukusanya mapato yatokanayo na utaifishaji wa madini hayo kama ilivyo kwa Wizara ya Maliasili kwa mazao ya misitu kama magogo na mkaa na pia Tra kwa bidhaa zinazoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru wa forodha.