Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan
Hali usalama wa raia na mali zao nchini imeelezwa kuwa ni mbaya kiasi cha kufikia hatua ya wahalifu kutamba mitaani, huku askari wa Jeshi la Polisi wakidaiwa kuwaogopa wahalifu hao na kufunga vituo vya Polisi kukimbilia maeneo wanayoona ni salama kwao.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, aliyasema hayo bungeni jana wakati akichangia mjadala uliohusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara.
Alisema hali ya usalama nchini ni mbaya kutokana na matukio yanayojitokeza kama vile vituo vya Polisi kuvamiwa na majambazi na kuporwa silaha, uwepo wa vikundi vya vijana wanaopiga na kupora wananchi mitaani maarufu kama 'Panya Road' na matukio ya ujambazi wa watu kutekwa na kuporwa mali zao, ambayo hivi sasa yamekithiri.
"Hali ya usalama wa raia na mali zao kwa sasa siyo nzuri, inatisha na inahitajika kazi ya ziada sana kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kuishi salama wao na mali zao…tulikuwa na vituo vidogo vya polisi mitaani na vimewekwa kwa makusudi kwa ajili ya kupambana na uhalifu mdogo mdogo mtaani, lakini hivi ninavyokwambia vituo hivi vimefungwa katika jimbo langu na katika Jiji zima la Dar es Salaam," alisema Azzan na kuongeza:
"Lakini katika hali inayojtokeza ya vituo kuvamiwa na majambazi na kuporwa silaha, sioni ajabu ya vituo hivyo kufungwa."
Ili kupunguza matukio ya uhalifu, Azzan alishauri majeshi mengine kama vile Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kulisaidia Jeshi la Polisi katika suala la usalama wa raia na mali zao.