Naibu Spika Job Ndugai.
Wananchi mbalimbali wamekuwa wakiuliza alipo Naibu Spika Job Ndugai, ambaye tangu kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge la Muungano hajaongoza kikao chochote kwani mara kadhaa chombo hicho kimekuwa kikitumia wenyeviti wakati Spika, Anne Makinda anapokuwa na majukumu mengine.
Ndugai, Mbunge wa Kongwa CCM, amekuwa akihudhuria vikao ambavyo baadhi huongozwa na wenyeviti, lakini tangu kuanza kwa wiki hii hajaonekana.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 6(2), (3) na (5), Naibu Spika atakuwa msaidizi wa Spika katika kuongoza Bunge na atatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni. Kanuni ya 6(3) inaeleza kuwa Spika anaweza wakati wowote bila kutoa taarifa rasmi kwa Bunge, kumtaka Naibu Spika au mwenyekiti kuongoza shughuli za Bunge.
Pia kanuni ya 6 (5) inampaka uwezo Naibu Spika kumtaka mwenyekiti wa Bunge kuongoza shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria bila ya kutoa taarifa rasmi kwa Bunge.
Alipotafutwa kwa simu, Ndugai, ambaye alionekana akiongoza vikao vya bunge kwa mara ya mwisho Novemba 20, mwaka jana wakati ulipotokea mjadala mzito kuhusu Bunge kujadili Ripoti ya Sakata la Escrow wakati kukiwa na kesi mahakamani, alisema alikuwa jimboni kwake Kongwa na kwamba atarejea leo.
Akizungumza kwa sauti ya chini tofauti na kawaida yake, Ndugai alieleza kuwa anasumbuliwa na tatizo la koo.
Alipoulizwa kama ana taarifa zozote za ugonjwa, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alikiri kupokea taarifa hiyo na kueleza kwamba aliaga kuwa anakwenda kuonana na daktari kuangalia afya yake.
Wakati wa Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge ambao ulishughulikia sakata la uchotwaji wa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, Ndugai aliweka msimamo madhubuti kuruhusu suala hilo kujadiliwa na chombo hicho licha ya kuwapo na zuio la Mahakama.
Akizungumza kwa kujiamini, Ndugai alisema Bunge litatenda haki katika suala hilo lililo lililohusisha mawaziri wanne na Mwanasheria Mkuu kabla ya kujadiliwa na kupitishwa maazimio manane.
Ndugai alitumia kauli ya Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta akisema: "Tukiwa viongozi hatuwezi kukubali kushikamana katika uozo."
Msimamo wake ulimfanya asifiwe na wabunge kutoka pande zote, wakimuelezea kuwa uamuzi wake utamfanya aingie katika historia ya nchi.
Kutoonekana kwake kwenye kiti cha Spika, kumekuwa mjadala hata kwa baadhi ya wabunge na jana mmoja wa wabunge wa NCCR-Mageuzi alieleza kuwa kutoonekana kwa mbunge huyo wa Kongwa kunatokana na ugonjwa baada ya kuulizwa na mbunge wa CCM.
Bunge la mwisho
Kutoonekana kwake wakati wa mjadala wa sakata la escrow, kulisababisha minong'ono mingi, lakini baadaye ilielezwa kuwa alikwenda Ulaya kwa shughuli za kikazi.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alitoa ufafanuzi wakati huo kuwa Ndugai alikuwa safarini Ufaransa kikazi, lakini alikanusha taarifa kuwa safari yake ilitengenezwa kutokana na msimamo wake kwenye sakata la escrow.
Katika sakata la escrow, zaidi ya Sh306 bilioni zilichotwa kwenye akaunti hiyo iliyofunguliwa kwa makubaliano kati ya Tanesco na kampuni ya IPTL inayoliuzia nishati shirika hilo la umma.
Pande hizo mbili zilitofautiana katika kiwango cha tozo na ndipo zilipokubaliana kufungua akaunti hiyo shauri lao likiwa mahakamani. Katika uamuzi wake, Mahakama ilizitaka pande hizo mbili kukokotoa upya tozo hiyo kabla ya kufanya malipo, jambo ambalo halikufanyika.
Wakati uamuzi wa kufanya malipo hayo kwa IPTL ukifanyika, Benki Kuu ilihoji kuhusu malipo ya kodi iliyotakiwa ilipwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema akashauri kufanyika kwa malipo hayo bila ya kukata kodi, jambo lililomfanya ajiuzulu.
Wengine walioondoka kutokana na sakata hilo ni Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati, Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kupisha uchunguzi dhidi yake. Tayari maofisa waandamizi watano kutoka TRA, Tanesco na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wamefikishwa mahakamani.