Friday, February 06, 2015

Pinda ashukiwa ndani na nje ya Bunge


Pinda ashukiwa ndani na nje ya Bunge
Kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa wanafunzi walioshiriki gwaride na halaiki kwenye sherehe za miaka 38 ya CCM mjini Songea ni watoto wa wanachama wa chama hicho, imekosolewa na wananchi na wabunge ambao walifikia uamuzi wa kuomba mwongozo.
Sherehe hizo zilifanyika Jumapili ya Februari Mosi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, zikishirikisha makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao walivalia sare za CCM na kuimba nyimbo za chama hicho huku wakicheza gwaride na halaiki, ambayo kwa kawaida huchukua muda mrefu kujifunza na kuielewa.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo, mtendaji huyo mkuu wa Serikali alitetea ushiriki wa watoto hao wapatao 500 kwenye sherehe hizo akisema ni sehemu ya mfumo wa wanachama wa CCM.
"Susan, utafikiri tulikuwa pamoja. Nilijua tu swali hili lazima litaulizwa. Ila 'mtoto wa nyoka ni nyoka'. Chama hiki kina mfumo wake ambao umeshuka mpaka kwenye ngazi ya kitu kinaitwa chipukizi," alisema akijibu swali la mbunge huyo aliyetaka kujua sababu za CCM kutumia watoto kwenye shughuli zake za siasa wakati ina wanachama wapatao milioni 10 kote nchini.
"Chipukizi hawa ni watoto ambao wamezaliwa kutokana na wazazi wana-CCM, ndiyo maana chama kiliwatumia. Sherehe ilikuwa nzuri na ilipendeza sana. Kwa kuwa hawajafikia umri wa kuingia katika masuala ya siasa, halina madhara lile rafiki yangu, pia bado ni wadogo mno na walikuwa wanafurahia gwaride na kuvaa sare tu."
Lyimo hakuridhishwa na jibu hilo la Waziri Pinda, akisema hakutakiwa kutoa majibu ya aina hiyo na kwamba katika mkusanyiko huo, kulikuwa na watoto ambao wazazi wao siyo wanachama wa CCM.
"Lengo la watoto hawa ni kusoma na siyo kufanya siasa. Iweje mfanye mambo kwa double standard (ndumilakuwili)?" alihoji na baadaye Pinda alitaka suala hilo lisiendelee kujadiliwa.
"Naheshimu maelezo ya Susan, lakini kiacheni chama kiendelee na utaratibu wake. Mfumo wake ndiyo huo, ndivyo ulivyo na sidhani kama kuna haja ya kuendelea kubishana katika suala hili," alisema Pinda ambaye ofisi yake inasimamia elimu ya msingi na sekondari.
Kabla ya nchi kuruhusu tena siasa za vyama vingi mwaka 1992, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walikuwa wakitumiwa kwenye shughuli za chama tawala na za Serikali, lakini imekuwa ni nadra kuonekana kwenye mikutano ya kisiasa tangu uhuru wa kidemokrasia ulipoanza.
Hata hivyo, ili kufanikisha sherehe hizo za CCM ambazo zilifanyika Jumapili kutokana na siku ya kuzaliwa chama hicho (Februari 5) kuwa katikati ya wiki, maofisa wa elimu ya sekondari wa Manispaa ya Songea walielezwa kuwaandikia barua wakuu wa shule zilizopo karibu na Uwanja wa Majimaji, wakiwataka kuhudhuria pamoja na walimu na wanafunzi ambao waliagizwa kuvaa sare.
Mkosamali aomba mwongoza
Majibu hayo hayakuwaridhisha wabunge wengine na baada ya kipindi cha maswali ya papo kwa papo, Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliomba mwongozo wa Spika juu ya suala hilo.
Mkosamali alisema kitendo cha kuwatumia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika sherehe hizo ni sawa na kuwalazimisha kukishabikia chama ambacho hawakipendi.
"Kuna barua zinaonyesha jinsi wanafunzi walivyolazimishwa kuvaa sare za chama na kuhudhuria sherehe hizo. Jambo hili siyo sawa kwa sababu linawalazimisha wanafunzi kuwa wanachama wa chama ambacho hawakipendi," alisema Mkosamali.
Spika Makinda alisema kuwa suala hilo lingetolewa ufafanuzi baadaye.
Wanasiasa, wasomi wazungumza
Baadhi ya wasomi walipinga kauli hiyo ya Waziri Mkuu kuhusu matumizi ya watoto kwenye shughuli za kisiasa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles Kitima alisema wanafunzi wanatakiwa kufundishwa uzalendo, tunu za taifa na historia ya nchi yao, lakini siyo itikadi za vyama vya siasa.
"Sasa tupo kwenye mfumo wa vyama vingi. Tulishaachana na mfumo wa chama kimoja ambao vijana waliandaliwa kukielewa chama tawala tangu wakiwa wadogo," alisema na kuongeza:
"Tunapaswa kujiuliza na vyama vingine vikifanya kama hiki kilichofanywa na CCM hali itakuwaje? Kilichofanywa na CCM ni makosa kwa sababu hata mzazi hutakiwi kumchagulia mtoto chama cha kukipenda. Mzazi anamrithisha mtoto mila na dini tu."
Alisema ushirikishwaji wa wanafunzi katika masuala kama hayo ndiyo chanzo cha watoto wadogo kuanza kutumika vibaya, akitoa mfano wa watoto wanaopigana vita Sudan.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Chris Peter Maina naye alitofautiana na maelezo ya Pinda akisema: "Si sahihi. Wanafunzi wanatakiwa kushiriki shughuli za kitaifa kama sherehe za uhuru au kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere. Kuwaingiza katika masuala ya kisiasa mapema kiasi hiki ni hatari."
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema inashangaza kuona kwamba hadi leo CCM wanadhani shule zote ni za chama hicho ndiyo maana wakaamuru walimu za wanafunzi kushiriki.
"Watoto wanatakiwa kufundishwa uraia na kusoma historia ya nchi yao na vyama vya siasa lakini siyo kuwashinikiza kukishabikia chama chochote. Hii inaonyesha wazi kuwa bado wenzetu wanadhani tupo katika mfumo wa chama kimoja cha siasa na ndiyo maana wanatumia vyombo vya dola kudhibiti karibu kila jambo linalofanywa na vyama vya upinzani.
"Kitendo kilichofanywa na CCM ni kuingilia haki ya watoto. Wanafunzi hawa wanatakiwa kuachwa wasome na kujichagulia mambo yao wenyewe."
Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Leticia Ghati alisema: "Kitendo walichokifanya si sahihi. Wanafunzi ni wa watu wote na huwezi kusema kuwa wote walioshiriki katika sherehe hizo ni watoto wa makada wa chama chao. Huu si mfumo mzuri wa utawala bora."