Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, (pichani) jana aliongoza umati wa wakazi wa Manispaa ya Dodoma kumuaga askari Polisi, Koplo Joseph Swai (27), aliyeuawa wakati akitekeleza majukumu ya kumuokoa mtoto aliyetaka kuchinjwa na baba yake mzazi na kuwataka askari kubuni mbinu mpya kila siku za kupambana na uhalifu na wahalifu.
Askari huyo alisafirishwa jana kwenda kwao Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa maziko.
IGP Mangu alisema Jeshi la polisi linatakiwa kuongeza kasi ya kupambana na uhalifu kutokana na kuongezeka kwa vitendo hivyo ndani ya jamii.
"Kijana amekufa kishujaa wakati akitetea mtu asiye na uwezo wakati akinyanyaswa, katika kifo hiki askari wapate cha kujifunza kwani kimewatia nguvu na kuwawezesha kufahamu namna ya kukabiliana na uhalifu.
Alisema msiba huo ni fursa ya kujihami na kukomesha uhalifu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa, alisema ni wajibu wa jamii kufichua wahalifu ili waweze kukabiliana na mikono ya sheria.
"Ni wakati wa kuanza kushughulika na cheche kwa kila mtu kuwajibika kwenye eneo lake na kuhakikisha usalama unakuwapo," alisema.
Wakati huo huo, kijana Tissi Mallya (29), wa Chang'ombe Juu, Manispaa ya Dodoma aliyemuua askari Swai, naye amefariki dunia baada ya wananchi wenye hasira kumpiga na kumjeruhi vibaya.
PC Swai aliuawa juzi wakati akimwokoa mtoto wa miezi minane, Valerian Mallya, aliyekuwa akiteswa na baba yake mzazi (Mallya), katika mtaa wa Chang'ombe Juu mjini hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema baada ya tukio la kuuawa kwa askari, polisi walianza msaka wa kumtafuta mtuhumiwa huyo na majira ya saa 5:00 usiku walipata taarifa kuwa wananchi wamemuona maeneo ya Mti Mkavu, Maili mbili akiwa bado na panga alilolitumia kumua askari.
Kamanda Misime alisema wananchi hao walichukua sheria mkononi na kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake hadi Polisi walipofika walimkuta akiwa mahtuti.
Alisema Polisi walimchukua mtuhumiwa huyo akiwa katika hali mbaya na kumkimbiza hospitali lakini baada ya kumfikisha daktari aligundua kuwa ameshafariki.
Aidha, alisema kumbukumbu za polisi zinnaonyesha kwamba mwaka 2006, mtuhumiwa huyo aliwahi kufungwa jela miaka mitatu kwa kosa la kujeruhi na mwaka 2009 alifungwa tena miezi sita kwa kosa la kutishia kuua.
PC Swai ameuawa juzi kwa kukatwakatwa kwa mapanga wakati akimwokoa mtoto wa miezi minane, aliyekuwa akiteswa na baba yake mzazi ambaye naye aliuawa baada ya kutenda unyama huo.