Saturday, June 21, 2014

HII SASA NI HATARI, MAJENEZA SASA KUTOZWA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI (VAT).




HII SASA NI HATARI, MAJENEZA SASA KUTOZWA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI (VAT).
Katika mkakati wake wa kuhakikisha inakusanya kodi ipasavyo, Serikali imependekeza kutoza kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), katika maeneo mbalimbali, ikiwamo uuzaji wa majeneza.

Katika miaka ya karibuni, biashara ya majeneza imekuwa kwa kasi kubwa, hasa Dar es Salaam.

Pendekezo hilo limo katika Muswada wa Sheria ya VAT unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni kuanzia Juni 27, mwaka huu, ambao pia umependekeza kutoza kodi hiyo katika maeneo mengine ya usindikaji maziwa, makandarasi wazawa na sekta ya utalii.

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema jana kuwa: "Ngoja tusikilize wadau wanasemaje, lakini  lengo la Serikali ni kukuza uchumi na kukusanya mapato."

Alisema kuondoa misamaha ya kodi si njia pekee ya kuvutia uwekezaji na kusisitiza kuwa nchi lazima ipate fedha ili kupeleka huduma kwa wananchi.

Juzi, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ilikutana na Kamati ya Bunge ya Bajeti, Wizara ya Fedha pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujadili muswada huo na kutoa maoni yao, huku wabunge wengi wakiupinga na kutaka uboreshwe.

Baadhi ya wadau wa sekta binafsi walimweleza Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge kuwa  licha ya muswada huo kutakiwa kufanyiwa marekebisho, hata wao hawakushirikishwa ipasavyo kwa maelezo kuwa waliuona Novemba mwaka jana na kupewa wiki moja tu ya kuujadili na kutoa maoni yao.

Kwa masharti ya kutotajwa majina, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti walisema ni jambo la ajabu kwa Serikali kuanza kukusanya kodi hadi katika uuzaji wa majeneza.

"Wameona biashara hii inafanywa na idadi kubwa ya watu sasa wanataka kuanza kutoza kodi ya VAT, huku si kuwatendea haki Watanzania, hata kama ni kupata mapato lakini si kwa njia hii."

"Muswada huu umekaa kisiasa zaidi, yaani kukusanya mapato tu, bila kutazama athari zake," alisema mmoja wa wajumbe hao.