Friday, October 10, 2014

WANAHABARI WA MATAIFA MBALIMBALI WATEMBELEA KITUO CHA VIUNGO BANDIA VYA BINADAMU INDIA


WANAHABARI WA MATAIFA MBALIMBALI WATEMBELEA KITUO CHA VIUNGO BANDIA VYA BINADAMU INDIA
Na Hassan Hamad - India. 
Kiasi cha wagonjwa 65,000 wenye ulemavu wa aina tofauti wanapatiwa visaidizi pamoja na matibabu kila mwaka nchini India, hatua ambayo huwawezesha kuendelea na shughuli zao za kimaisha kama kawaida. 
Meneja wa kituo kikuu cha viungo bandia vya binadamu katika mji wa Jaipur jimbo la Rajasthan kaskazini mwa India, Om Prakash Sharma ameeleza hayo mbele ya waandishi wa habari kutoka baadhi ya nchi za Afrika, Asia na Latin America waliofika kituoni hapo hivi karibuni kwa ziara maalum ya kimasomo. 
Sharma amesema kituo hicho kijulikanacho kwa jina la "Bhagwan Mahaveer Viklang Sahayata Samiti (BMVSS), ndio kituo kikubwa zaidi duniani kinachojihusisha na utengenezaji na utoaji wa viungo bandia vya binadamu vikiwemo miguu na mikono. 
Amesema mara mgonjwa anapofika kituoni hapo au tawi lolote la kituo hicho miongoni mwa matawi 23 yaliyoko nchini India, hufanyiwa vipimo na baada ya siku chache hupatiwa viungo anavyohitaji bila ya malipo, ambavyo humuwezesha kuendelea na shughuli zake kama ilivyokuwa awali baada ya muda mfupi. 
"Mara baada ya mgonjwa kupatiwa viungo anavyostahiki hufanyishwa mazoezi na baada ya siku chache tu anaweza kufanya shughuli zake za kimaisha ikiwa ni pamoja na kushiriki katika masuala ya kiuchumi pamoja na michezo", alieleza Sharma na kuongeza; "Viungo vinavyotengenezwa na kituo hiki ni imara na vyenye viwango vya hali ya juu, na vinatengezwa kisayansi. Vinaweza kudumu hadi miaka sita au kumi bila ya kufanyiwa matengenezo ya aina yoyote". 
 Amefahamisha kuwa mara nyingi wagonjwa wanaofika kwenye kituo hicho ambacho pia hujulikana kwa jina la "Jaipur Foot Knee/Limb" pamoja na matawi yake, ni wale waliopata ulemavu wa viongo kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kimaumbile, ajali za barabarani, matukio ya vita na maradhi mbali mbali yakiwemo polio. 
Sharma ameeleza kuwa kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1975 kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa wanaopoteza viungo kutokana na sababu mbali mbali hasa watu wa daraja la chini, kilianza kwa kutengeneza na kutoa miguu na mikono bandia 59, ambapo hadi kufikia katikati ya mwaka huu tayari kimewahudumia watu wapatao milioni moja na laki nne (1.4 million), ambao ni wastani wa watu 50,000 hadi 65,000 kwa mwaka. 
Ameongeza kuwa mbali na wagonjwa kupatiwa viungo hivyo, baadhi yao wamekuwa wakipatiwa visaidizi vyengine vikiwemo vigari na baiskeli ambavyo huwasaidia kuendeleza harakati zao za kimaisha ikiwa ni pamoja na kufanya biashara mbali mbali. 
Pia baadhi yao wamekuwa wakipatiwa misaada ya fedha na vitendelea kazi kwa masharti nafuu. Katika jitihada za kuwasaidia wananchi hasa wa kiwango cha chini, Sharma amesema baadhi ya watendaji hulazimika kusafiri katika maeneo tofauti yaliyokumbwa na majanga yakiwemo vita ndani na nje ya India, ambako hufungua kambi katika maeneo hayo na kutoa huduma za kimatibabu kwa waathirika. 
Amesema hadi kufikia mwaka 2014, tayari wametoa huduma katika kambi zipatazo 26 katika nchi mbali mbali zikiwemo Afghanistan, Philippines, Nigeria, Sudan, Rwanda na Kenya. Mohamad Sehebay kutoka mji wa Uttar Pradesh aliyefika kituoni hapo kwa ajili ya marekebisho ya mguu wake wa bandia, aliwaambia waandishi hao kuwa amekuwa akiutumia mguu huo kwa kipindi cha miaka sita mfululizo bila ya matatizo yoyote. 
"Nilipata ajali ya barabarani mwaka 2008 na baada ya kupata taarifa za kituo hiki nilikuja hapa, na nashkuru nilipatiwa mguu bandia na unanisaidia sana. Tayari nilikuwa nimeshakata tamaa na maisha lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa msaada wa kituo hiki nimeendelea kuishi kwa matumaini makubwa", alisema Mohamad huku akionesha uso wa bashasha. 
Wazo la kuanzishwa kituo hicho kinachofanya kazi kama taasisi binafsi (NGO), lilikuja baada ya bwana D.R.Mehta ambaye ni mwanzilishi wake kupata ajali mbaya ya barabarani, na kuungwa mkono na madaktari wawili waliompatia matibabu, wote kutoka hospitali ya Mahatma Gandhi, Jodhpur nchini India.
Waandishi wa habari kutoka nchi mbali mbali wakiangalia viungo bandia vya binadamu, walipotembelea kituo kikuu kinachotengeneza viungo hivyo nchini India.
Waandishi wa habari kutoka nchi mbali mbali wakiangalia viungo bandia vya binadamu, walipotembelea kituo kikuu kinachotengeneza viungo hivyo nchini India.
Waandishi wa habari kutoka nchi mbali mbali wakiangalia viungo bandia vya binadamu, walipotembelea kituo kikuu kinachotengeneza viungo hivyo nchini India.
Meneja wa kituo kikuu cha viungo bandia vya binadamu katika mji wa Jaipur nchini India, OM Prakash Sharma akionyesha mguu bandia wakati waandishi wa habari kutoka nchi mbali mbali walipofika kituoni hapo kwa ziara ya kimasomo. Picha kwa hisani ya Hassan Hamad-India