Na Allan Ntana, Sikonge
MWENYEKITI wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora Robert Kamoga amepongeza jitihada zinazofanywa na mradi wa PROSPER katika kutokomeza utumikishwaji watoto katika shughuli za kilimo huku akisifu utaratibu wa kurudishwa shule watoto wote waliokosa nafasi hiyo.
Kamoga ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya kupinga utumikishwaji watoto iliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Udongo kata ya Ipole wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Alisema mradi huu unastahili kupongezwa kwa sababu mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa 5 inayoongoza kwa umaskini hapa nchini na asilimia kubwa ya wananchi wake ni maskini hali inayochangia watoto wengi kutumikishwa katika kazi ngumu kwa ujira mdogo.
Mradi huu ni mkombozi kwa watoto wadogo kwa sababu wazazi wengi walikuwa hawawapeleki shule kwa kisingizio cha umaskini na badala yake wanawapeleka shambani wakawasaidie kulima tumbaku au kuchunga ng'ombe, alisema.
Kamoga aliongeza kuwa utumikishwaji watoto ni hatari sana katika ustawi wao kwa sababu huwakosesha fursa mbalimbali katika makuzi yao ikiwemo haki ya kupata elimu na malezi bora. "Wataalamu wanasema ukimnyima mtoto haki zake anaathirika kisaikolojia mpaka ukubwani mwake na watoto ndio taifa la leo na kesho, hivyo wanapaswa kulindwa, kutunzwa na kupendwa, kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajenga taifa kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa, alifafanua.
Aidha alisema sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 78 (1) inakataza mtu yeyote kuajiri au kutumikisha watoto katika shughuli yoyote ile inayowaadhili watoto hao, hivyo kumtumikisha ni kwenda kinyume na sheria za nchi anapaswa kushitakiwa mara moja.
Kamoga alisema PROSPER imefanikiwa kuwarudisha shuleni watoto wengi sana waliokosa elimu katika wilaya za Sikonge na Urambo na kuwagharamiwa masomo yao kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba huku vikundi mbalimbali vya vijana na akina mama vikipewa mafunzo ya ujasiriamali, kilimo, ufugaji na mikopo kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Mradi huu umefanya kazi nzuri sana katika vijiji 20 vilivyoko katika wilaya hizo, Mkurugenzi (Bahati Nzunda) naomba uangalie uwezekano wa kupanua huduma hii katika vijiji vingine kwani wapo watoto wengi sana walioathiriwa na utumikishwaji huu, aliongeza.
Ili kudhibiti vitendo hivyo, Kamoga aliagiza waalimu wakuu wa shule zote za msingi katika wilaya hiyo kuhakikisha wanafuatilia mahudhurio ya watoto shuleni ili kubaini watoto wasiofika shule ili wazazi wao wakamatwe mara moja na kutozwa faini.
Sambamba na hilo aliagiza watendaji wote wa halmashauri kuanzia ngazi ya vijiji na kata kuwachukulia hatua kali watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya utumikishwaji watoto katika maeneo yao huku akiomba asasi zingine kuunga mkono jitihada hizo.
BW.ROBERT KAMOGA (WA KWANZA KULIA) MWENYEKITI WA HALMASHAURI SIKONGE AKIWA NA MKURUGENZI WA MRADI WA PROSPER BAHATI NZUNDA (WA KWANZA KUSHOTO) AKIFUATIWA NA DR MTIBA NA MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA URAMBO ADAM MALUNKWI.JPG
ROBERT KAMOGA AKIHUTUBIA UMATI WA WANANCHI WA VIJIJI VYA UDONGO NA MAKAZI KATIKA KATA YA IPOLE WILAYANI SIKONGE MKOANI TABORA KATIKA MAADHISHO YA SIKU YA KUPINGA UTUMIKISHWAJI WATOTO KATIKA MASHAMBA YA TUMBAKU.JPG