Sunday, June 28, 2015

WASAFIRISHAJI WA MADAWA YA KULEVYA WABUNI MBINU MPYA KUSAFIRISHA MADAWA HAYO


WASAFIRISHAJI WA MADAWA YA KULEVYA WABUNI MBINU MPYA KUSAFIRISHA MADAWA HAYO


Wakati Tanzania ikianza kutumia sheria mpya kwa washukiwa wa dawa za kulevya inayomhukumu mshtakiwa kifungo cha maisha jela, wafanyabiashara wa madawa hayo wamebuni mbinu mpya ya kusafirisha dawa hizo kwa kutumia taulo lililolowekwa kwenye dawa hizo.



Wafanyabiashara hao wanaposafirisha dawa hizo kama heroine au cocaine huziweka kwenye mfumo wa kimiminika kisha taulo wanalidumbukiza kwenye maji ya dawa na kuanika kwenye jua.

Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzoa, alisema hayo katika mahojiano maalum na NIPASHE Jumapili.

Alisema taulo husafirishwa kama nguo nyingine na wanapofika nchi husika huliloweka kwenye maji na kulikamua ili kutoa dawa hizo.

Alisema mbinu hiyo ilibainika kupitia mkutano uliofanyika nchi ya Seychelles wiki iliyopita ambapo moja ya washirika kwenye mapambano hayo aliielezea kama changamoto mpya.

Alisema ingawa hakuna mtu aliyekamatwa kwa kutumia mbinu  hiyo Tanzania, imebainika kwenye moja ya nchi wanazoshirikiana nazo dhidi ya mapambano hayo hutumika.

Kamanda Nzoa alisema wamekuwa na ushirikiano na nchi nyingine kwenye mapambano ya dawa za kulevya ambayo sasa yamezaa matunda baada ya usafirishaji kupungua.

Alisema mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano mingine inayofanyika kila mara yenye lengo la kubadilishana mikakati ya mapambano ambayo mafanikio yake yalionekana toka mwaka uliopita.

Alitaja mbinu nyingine inayoendelea kutumiwa kuwa ni usafirishaji wa vibashirifu ambavyo ukamataji wake huhitaji kutumia mbwa.

Alisema baada ya Mtanzania kukabilia na kesi za namna hiyo, walizungumza na Afrika Kusini ambapo wengi huvipeleka huko ili nao wabadili njia za ukamataji.

Alisema mbinu nyingine ni kubadili uelekeo wa usafirishaji ambapo kama alikuwa anaenda Afrika Kusini atapita nchi nyingine kupoteza ushahidi na kwenda alikokusudia.

Kuhusu sheria mpya, Kamanda Nzoa alisema, itaanza kutumika wakati wowote ambapo mshitakiwa atakapokutwa na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha.

Kamanda Nzoa alisema Rais Jakaya Kikwete, ameshaisaini sheria hiyo na itawahusu wenye tabia ya kuwakodishia nyumba wafanyabiashara wa dawa za kulevya, ambao mara baada ya kukamatwa hudai hawajui chochote.

Alisema baada ya changamoto nyingi kujitokeza dhidi ya vita hiyo, wameamua kubadilisha sheria.

"Sheria ya sasa tofauti na mwanzo, itakuwa haionyeshi thamani ya mzigo aliokutwa nao mhusika, mzigo uwe mdogo au mkubwa wote kifungo ni cha maisha jela," alisema.

Alifafanua, tofauti nyingine ya sheria ya sasa na ya zamani, hii mpya imeongezwa vibashirifu vya kutengenezea dawa hizo ambavyo ni  moja ya mbinu za wasafirishaji zinazotumika kusafirisha dawa hizo.

Alisema kwa ujumla hali ya dawa za kulevya kidunia ikiwamo Tanzania, ni nzuri kutokana na mtandao mpana waliokuwa nao dhidi ya mapambano.

Kuhusu takwimu za ukamataji, Kamanda Nzoa, alisema mwaka jana katika ukanda wa bahari walikamata kilo 241 za dawa hizo na mwaka huu jumla ya kilo 48 za heroine zimekamatwa ndani ya nchi.

Alisema wamekamata kilo 981 za dawa za kulevya aina ya Heroine Bahari Kuu ambazo ziliteketezwa huko huko.

"Kiwango hiki kilichokamatwa mwaka huu maana yake ni kwamba wale wanaotumia Heroine kwa sasa Tanzania hali zao ni mbaya kwa maana kuna upungufu mkubwa," alisema.

Alisema ushirikiano walionao na nchi nyingine umesaidia, idadi ya majahazi yaliyokuwa yakitumika kusafirishia dawa hizo kupungua.

Kuhusu bajeti iliyotengwa kwenye eneo hilo Kamanda Nzoa alisema ofisi yake haiingalii sana kwa sababu, mapambano kati ya nchi na nchi yanahitaji mawasiliano ya simu ambayo gharama zake sio kubwa.

"Tukiangalia sana bajeti kazi zetu zitalala, kitu tunachoangalia ni ushirikiano kati ya nchi hizi na kubadilishana uzoefu kupitia mikutano mbalimbali tunayoitisha," alisema.