Sunday, June 28, 2015

Watu sita wanaodhaniwa kuwa Raia wa Comoro waokotwa wakiwa hai baada ya kukaa baharini kwa siku 45



Watu sita wanaodhaniwa kuwa Raia wa Comoro waokotwa wakiwa hai baada ya kukaa baharini kwa siku 45


WATU sita wanaodhaniwa kuwa ni wavuvi raia wa Comoro, ambao wameondoka kwao tokea Mei 11 mwaka huu na kukaa baharini wakiwa na chombo chao siku 45, wameokotwa jana katika bahari ya Matumbulini wilaya ya Mkoani Pemba.


 Watu hao waliokotwa na wavuvi wa shehia ya Mwambe wilayani humo, wakati walipokuwa kwenye kazi zao za uvuvi, ndipo waliopoona ishara ya nguzo zikipeperuka baina ya majira ya saa 4:00 na saa 5:00 usiku na walipowafika walikuta watu hao kutoka Comoro.

Taarifa zinaeleza kuwa baada ya kuokotwa wakiwa wanaelea elea na chombo chao aina ya 'Fiber' walifikishwa hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani majira ya saa 6:00 usiku na kuanza kutiwa majia na kisha kufanyiwa uchunguuzi wa afya zao.

Akizungumza na waandishi wa habari hizi hospitali hapo, Muuguzi wa afya ya akili wa hospitali hiyo, dk Said Ali Said alikiri kuwapokea watu hao, ambapo alisema baada ya uchunguuzi wamegundua kuwa walikuwa wamekosa nguvu baada ya kukosa chakula.

"Unajua tumegundua kuwa, wamekosa nguvu mwilini, maana wamekaa na njaa kwa muda mrefu, ingawa samaki wa kukausha kwa jua waliokuwa wanakula, kidogo wamewasaidia kwa hivyo hakuna alieathirika'',alifafanua.

Alifafanua kuwa mara baada ya kuwatia maji, waliwapatia uji, chai na mikate, ambapo afya zao zilianza kujirudia kama kawaida na kwa sasa wanaendelea vyema.

Aliwataja watu hao waliojiita wavuvi kuwa ni, nahoza Alloui Huomad Mromaji (40), msaidizi nahoza Yunus Maishe Mussa (45), Deiyan Ahamad Wali (25), Hassan Mmadi Abdul (59), Ibrahim Mzee Said (45) na Abdalla Abdurr-ahaman Abass (35) wote wakaazi wa visiwa vya Comoro.


Akizungumza na waandishi wa habari msaidizi nohoza wa wavuvi hao ambae anazungumza lugha ya kiswali kidogo, Yunus Maishe Mussa, alisema hawakuwa katika mavuvi siku hiyo, bali walikumbwa na mkasa huo walipokuwa wakirudi kununu chakula.

"Hii ni boti yetu ya uvuvi, lakini hiyo tarehe hiyo 11 ,wezi Mei, tulikuwa tunatoka kisiwa kimoja kwenda chengine, ndipo tulipoishiwa na mafuta na kubururwa na maji hadi Pemba'',alifafanua.

Alieleza kuwa hawakuja kisiwani Pemba kwa nia mbaya, bali ni kutokana na upepeo unavyo vuma, ndio maana wamejikuta kisiwani humo jana, baada ya kukaa baharini siku 45 na kuokotwa na wavuvi wenzao.

"Kipindi chote hicho tulikuwa tunakausha samaki kwa jua, na kisha tunakula, ndio chakula chetu hatuna chengine, hadi tullipoletwa juu bandari ya Mkoani'',alifafanua.

Afisa Uhamiaji wilaya ya Mkoani Pemba Abdalla Shehe alisema, wanaendelea kufuatilia taarifa za watu hao, kwanza kujua iwapo ni wavuvi na baada ya kujiridhisha watawakabidhi kwa ubalozi mdogo wa Comoro uliopo Zanzibar kwa kuwarejesha kwao.

Hata hivyo alisema wanamashaka kidogo kwa vile kama ni wavuvi walipaswa waone sehemu maalumu ya kuhifadhia samaki, na kukosekana ndani ya chombo hicho, ndio maana hawajaridhishwa na kauli zao.

"Tunafanya mawasiliano ya kimataifa, kujua kwamba kwenye nchi yao kuna taarifa za kupotea wao, na kisha na sisi baada ya uchunguzi wetu kukamilika na kujiridhisha tutawasiliana na ubolozi kwa hatua'',alifafanua.


Hii ni mara ya pili ndani ya mwaka huu kwa wavuvi kutoka Comoro kuokotwa bahari ya Mkoani kwa madai ya kubururwa na upepo ambapo mwezi uliopita waliokotwa wavuvi wawili.

CRD: ZANZIBAR NEWS