Bagamoyo ni mji mwambanoni wa Bahari Hindi katika Tanzania takriban 75 km kaskazini ya Dar es Salaam na km 45 magharibi ya kisiwa cha Unguja.
Bagamoyo iko kati ya miji ya kale kabisa ya Waswahili katika Tanzania. Maghofu ya Kaole (msikiti na makaburi ya karne ya 13 BK) yako karibu na Bagamoyo yakionyesha umuhimu wa utamaduni wa Kiislamu katika eneo hili.
Lakini hakuna uhakika kuhusu historia ya Bagamoyo ya kale isipikuwa ya kwamba mnamo karne ya 18 mji haukuwa muhimu. Wakazi walio wengi wakati ule walikuwa wavuwi na wakulima, palikuwa na biashara kiasi cha samaki na chumvi.
Mlango wa misafara ya Afrika ya Kati
Mwisho wa karne ile familia za Waarabu kutoka Oman walihamia Bagamoyo wakipanusha biashara yake. Mji ukawa kituo muhimu zaidi kwenye pwani; biashara ya misafara mikubwa ya karne ya 19 kwenda barani hadi Kongo ilianza na kurudi hapa.
Bandari wa watumwa
Hii ni sehemu (jela) ya watumwa waliokuwa wakihifadhiwa kabla ya kupelekwa kuuzwa sehemu mbalimbali.
Hasa kuhamia kwa makao ya Sultani wa Oman kuja Zanzibar kuliongeza umuhimu wa mwambao karibu na Unguja. Wafanyabiashara wa Zanzibar walikusanya bidhaa zao huko Unguja wakavuka bahari na kuajiri mahamali. Wakarudi miezi au miaka kadhaa baadaye wakileta pembe za ndovu na watumwa. Kwa njia hiyo Bagamoyo ilijulikana kama bandari kuu ya biashara ya watumwa kwenye pwani la Afrika ya Mashariki katika karne ya 19. Watumwa wakasafirishwa kwa jahazi au dhau hadi Unguja wakiuzwa huko sokoni.
Ngome ya ujerumani Bagamoyo katika karne ya 19.
Mapadre wa Roho Mtakatifu walijenga kituo chao cha kwanza katika Afrika ya Mashariki huko Bagamoyo wakiona umuhimu wa mji kama mlango wa bara.
Bagamoyo katika miaka ya 1890
Mji mkuu wa koloni ya Kijerumani
Aprili 1888 Sultani wa Zanzibar alikodisha eneo la pwani kwa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki walioanzisha makao makuu yao Bagamoyo. Ukali wa kampuni ulisababisha katika muda wa wiki chache ghasia ya wenyeji wa pwani yaliyokuwa vita ya Abushiri ikakandamizwa na wanajeshi wa Ujerumani. Mwaka 1890 serikali ya Ujerumani ilichukua madaraka ya utawala badala ya kampuni halafu mji mkuu ukahamishwa Dar es Salaam.
Umuhimu wa Bagamoyo ilianza kupungua tena kwa sababu meli kubwa zilitumia bandari ya Daressalaam badala ya Bagamoyo.
Mji wa kisasa
Leo hii Bagamoyo ni mji mdogo. Majengo yake ya kihistoria yako katika hali mbaya. Wakazi walio wengi wanaishi katika sehemu jipya la Magomeni na soko jipya. Majaribio ya hifadhi la urithi wa kihistoria hayakufaulu miaka mingi.
Bagamoyo ina chuo cha kitaifa ni Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo.
Tangu 2002 barabara ya lami imepatikana na kuleta matumaini ya kuongezeka kwa utalii. Kuna ombi la kuingiza Bagamoyo katika orodha ya UNESCO ya Urithi wa Dunia (World Heritage).