Monday, December 07, 2015

KATIBU MKUU, WIZARA YA ARDHI AFANYA JITIHADA KUBORESHA MABARAZA YA ARDHI NA NYUMBA YA WILAYA



KATIBU MKUU, WIZARA YA ARDHI AFANYA JITIHADA KUBORESHA MABARAZA YA ARDHI NA NYUMBA YA WILAYA
Katibu Mkuu wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Alphayo J.Kidata, amefanya ziara katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na kufanya maboresho, pamoja na kuahidi maboresho zaidi. 
Mhe. Kidata amefanya ziara hiyo ya ghafla katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya za Kinondoni na Ilala ili kubaini uendeshaji wa kazi katika Mabaraza hayo. Akisomewa ripoti fupi na mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kinondoni, Bw. Yose Mlyambina pamoja na mambo mengine alisema; "Kumekuwa na tatizo la kuhofia usalama wa majalada, kutokana na kuwa na vitasa vibovu katika baadhi ya milango". 
Aliendelea kueleza baadhi ya matatizo mengine katika baraza hilo ni ukosefu wa umeme, ambao ulihitaji kulipiwa, mafunzo kwa watumishi, kompyuta, gari la kutembelea katika maeneo ya migogoro, uhaba wa watumishi, stationaries na mazingira bora ya kazi. 
 Kwa upande wake msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Bi.Bahati Mlole alikiri kuwepo kwa matatizo hayo na kumtaka mwenyekiti wa Baraza la Kinondoni kujitahidi kutoa mafunzo muhimu ya awali kwa watumishi wa Baraza hilo, ikiwa ni moja ya njia ya kuboresha utendaji wa kazi katika baraza hilo. Hata hivyo Mhe. Kidata aliahidi kumaliza tatizo la vitasa vibovu kwa kuvinunua yeye mwenyewe kwa mshahara wake, alitoa pia kiasi cha Tsh.100,000 kwa ajili ya malipo ya umeme, alitoa kompyuta mbili ambazo zilikuwa ofisini hapo baada ya kuazikimwa tu kutoka Wizarani. 
Vile vile Kidata aliahidi kuwapatia gari, pamoja na kuwaongezea watumishi, na kuahidi kuboresha mazingira ya eneo la Baraza hilo ambayo yalikuwa hayaridhishi kiafya. 
Akiwa katika baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Ilala lililopo katika jengo la Mwalimu House – Ilala; Bw. Kidata akiongea na mwenyekiti wa baraza (Bi. Mwendwa Mgulambwa) na Watumishi wa baraza hilo, alisifia mazingira bora ya Baraza hilo na kuahidi kutatua tatizo la upungufu wa samani lililokuwa tatizo zaidi katika Baraza hilo. 
 Aidha Bw.Kidata aliahidi kusimamia kidete suala la malimbukizo ya madeni ya posho za wazee wa mabaraza hayo na kuahidi ifikapo Ijumaa tatizo hilo litakuwa limekwisha.
 Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Alphayo J. Kidata, akipekua baadhi ya majalada katika chumba cha majalada ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Kinondoni alipofanya ziara katika baraza hilo.
 Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.  Alphayo J. Kidata, akionyeshwa na Mwenyekiti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya - Kinondoni, Bw. Yose Mlyambina kompyuta zilizoazimwa kutoka Wizarani, kutokana na ufinyu wa vitendea kazi hivyo. Hata hivyo Kidata alitoa ruhusa kwa Mwenyekiti kuchukua Kompyuta hizo moja kwa moja kwa ajili ya matumizi ya Baraza hilo alipofanya ziara katika baraza hilo.
 Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Alphayo J. Kidata, akitoa Tsh. 100,000 kwa Karani kwa ajili ya matumizi ya malipo ya umeme kwa baraza la ardhi na nyumba ya wilaya la Kinondoni alipofanya ziara katika baraza hilo na kubaini baraza hilo kukosa umeme kutokana na kutopata pesa za malipo hayo

Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Alphayo J. Kidata, akieleza kwa Mwenyekiti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya - Kinondoni, Bw. Yose Mlyambina na ujumbe alioambatana nao kutoka Wizarani, kuhusu kuboresha mazingira ya eneo la baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Kinondoni, alipofanya ziara katika baraza hilo.