Wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar wamehimizwa kuwa tayari kufanya kazi popote watakapopangiwa ambapo watakuwa na wajibu wa kuthamini na kuchangia jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kupambana na maradhi mbali mbali yanayoisumbua jamii Nchini.
Himizo hilo limetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kwenye Mahafali ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar yaliyofanyika kwenye Kampas ya chuo hicho yaliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Jumla ya wahitimu 440 wa kada saba walihitimu na kufanikiwa kupata stashahada mwaka huu wa masomo kukiwa na ongezeko kubwa mara mbili ikilinganishwa na wahitimu 280 wa mwaka 2014.
Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein ambae Hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idii alisema wapo baadhi ya baadhi ya wahitimu wanaoajiriwa na Wizara ya Afya wanapiga chenga kufanya kazi Kisiwani Pemba wakisahau kwamba Wananchi wa kisiwa hicho wanahitaji kupata huduma zao.
Alisema watumishi wa Umma wakiwemo wa sekta ya afya wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi na miongozo ya sehemu wanazoajiriwa na inapendeza zaidi wawe mfano wa tabia njema kwa kushikamana katika kutekeleza maadili ya kazi zao.
Aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar kwa kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya Serikali tokea kilipoanzishwa katika kuimarisha sekta ya afya kwa misingi iliyowekwa na waasisi wa Afro Shirazy Party wakati wa kupigania uhuru wa Nchi hii. Mmoja wa wahitimu hao Faika Karim Zam kwa niaba ya wenzake wameuomba Uongozi wa Chuo hicho kuanzisha mafunzo ya ngazi ya Shahada { Diploma } kwa nia ya kuwapunguzia gharama za kutafuta elimu hiyo nje ya nchi.
Mapema Mkuu wa Chuo cha Taalum za Sayansi za Afya Zanzibar Dr. Haji Mwita Haji alisema Uongozi wa Chuo hicho kupitia Baraza lake umeamua kuongeza majengo zaidi ili kuwahudumia vyema wanafunzi wanaoamua kujiunga na chuo hicho sambamba na mahitaji ya ongezeko la Hospitali na vituo vya Afya Nchini.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufungaji wa Mahafali hayo ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo aliwaomba wauguzi kufuata maadili ya kazi zao ili kupunguza au kuondosha kabisa malalamiko yanayotolewa na wananchi.
Mh. Mahmoud alisema lugha zao kwa wagonjwa ndio kitendo kilichompa wakati mgumu alipokuwa akijibu maswala ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Vikao vya Baraza hilo vilivyokuwa vikiendelea kwa muda wote wa miaka mitano iliyopita.
Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya fani ya Uuguzi wakisubiri kuhudhurishwa baada ya kumaliza mafunzo yao ya miaka Mitatu katika chuo cha Taaluma za Sayanasi za Afya Mbweni.
Wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya fani ya maabara wakifuatilia matukio mbali mbal;I yaliyokuwa yakiendelea kwenye mahafali ya kumaliza mafunzo yao hapo Mbweni.
Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya fani ya Uuguzi wakisubiri kuhudhurishwa baada ya kumaliza mafunzo yao ya miaka Mitatu katika chuo cha Taaluma za Sayanasi za Afya Mbweni.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Mbweni Dr. Abdulla Ismail Kanduru kushoto akiteta na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar kwenye mahafali ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afra Mbweni.
Balozi Seif akimkabidhi Cheti Maalum Salama Witi Asfau wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya akiwa Mhitimu bora wa Fani ya Usanifu wa Vifaa Tiba vya Hospitali kwa mwaka 2015.