Akizungumza , Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Hamis Chagonja alisema bajeti ya Sh341 bilioni ilikuwa imetengwa kwa ajili ya wanafunzi 14,226 wa mwaka wa kwanza.
Hata hivyo, alisema Serikali imeongeza fedha hizo hadi kufikia Sh473 bilioni ambazo zinatosha kuwalipa wanafunzi 52,000. Alisema ongezeko hilo litawawezesha wanafunzi wengine 37,774 ambao hawakuwamo kwenye bajeti kudhaminiwa na bodi yake kwa mwaka huu wa masomo.
"Kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao ni 71,125 hatuna shida sana, wao wataweza kupata fedha hizo. Changamoto ilikuwa kwa hawa wa mwaka wa kwanza, lakini sasa tumepata fedha za kuwalipa," alisema.