Ilitengenezwa na Jeshi la Wanamaji la Ujerumani na kukamilishwa mwaka 1906. Aprili 1914 meli hii ilipangiwa majukumu ndani ya Afrika Mashariki na ilisafiri kutoka Ujerumani hadi bandari ya Dar es Salaam ambako pia ilipangwa kuwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma mwaka 1914.
Ilikuwa ni meli kubwa yenye uwezo wa kukimbia kilometa 44.6 kwa saa ambao ulikuwa ni mwendo mkubwa sana kwa wakati huo. Ilikuwa na bunduki kubwa kumi na mabomba matatu makubwa ya kutolea moshi ndipo wenyeji walipoiita Manowari ya Bomba Tatu wakiitofautisha na meli nyingi za wakati huo zilizokuwa na mabomba mawili ya kutolea moshi.
Simulizi zinasema kuwa mara tu Konigsberg ilipotia nanga bandarini Dar es Salaam mji mzima ulizizima. Mamia ya watu walifurika pale Magogoni na sehemu za Kigamboni kuishangaa meli hiyo kubwa ya aina yake kwa wakati huo.
Hali ilikuwa hivyo kila ilipokwenda iwe Tanga, Bagamoyo, Lindi au Mtwara. Manowari ya Bomba Tatu ilikuwa ni kivutio cha aina yake. Kweli ilikuwa ni gumzo kila kona na alama ya nguvu za Wajerumani katika Afrika Mashariki.
Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilipozuka Julai 1914, Konigsberg ilijaribu kuharibu misafara ya biashara ya Uingereza na Ufaransa katika bahari ya Hindi.
Chini ya Unahodha wa Maxi Loof, mnamo tarehe 20 Septemba 1914, Konigsberg iliishambulia na kuizamisha meli ya kivita ya Uingereza HMS Pegasus katika mapambano ya Zanzibar.
Upungufu wa makaa ya mawe uliathiri ufanisi wa meli hii na kuifanya iweze kuzamisha meli moja tu ya kibiashara kwenye kampeni nzima ya Afrika Mashariki ambayo ni HMS City of Winchester.
Nahodha wa Königsberg aliamua kuificha meli yake kwenye delta ya mto Rufiji ili kuzifanyia matengenezo injini zake lakini kabla ya matengenezo kukamilika meli mbili za uchunguzi za Kiingereza ziitwazo Mersey na Severn ziliigundua Königsberg pale kwenye delta na kuiharibu kwa kuipiga kwa makombora.
Mnamo tarehe 11 Julai 1915, meli zile za Uingereza zilisogea karibu kabisa na kuiharibu vibaya Königsberg, hivyo nahodha wake Loof na askari waliosalia wakaamua kuiharibu Königsberg ili isiangukie mikononi mwa Waingereza.
Askari waliosalimika katika mapambano yale ya Rufiji Delta walichukua bunduki zake zote 10 na wakaungana na Kamanda wao wa vikosi vya ardhini Paul von Lettow-Vorbeck katika vita vya msituni vilivyodumu hadi mwisho wa Vita va Kwanza ya Dunia.
Kati ya mwaka 1963 hadi 1965 timu ya wataalamu waliibomoa Königsberg kwa ajili ya chuma chakavu na mabaki yake yakazamishwa chini ya mto Rufiji. Huo ukawa mwisho wa meli hii iliyoteka hisia za wengi Afrika Mashariki, hususan Tanzania ya wakati huo.
NA RAJAB KIPANGO