Shule ya Msingi Zanaki, iliyopo Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam imeendelea kuongoza kwa ubora kitaaluma kwa mwaka wa pili mfululizo baada kushika nafasi ya pili kwa darasa la saba kati ya shule 167 za msingi za serikali.
Pia Zanaki imeshika nafasi ya kwanza kwa ubora katika mitihani ya darasa la pili ikiongozwa na Msimbazi Mchanganyiko kwa shule zote za msingi katika manispaa hiyo.
Akitanganza ushindi wa Zanaki, Afisa Elimu Msingi wa Manispaa hiyo, Elizabeth Thowa, alisema shule hiyo imeendelea kuwa kinara kitaaluma baada ya wanafunzi wake kupata alama nyingi za A na B kwa masomo yote.
Alisema Zanaki imefanikiwa kushika nafasi ya 10 kwa ubora kitaaluma kwa kushirikisha shule zote za serikali na binafsi kwa darasa la saba, huku ikishika nafasi ya nne kwa ubora wa mitihani ya darasa la nne kwa shule zote.
Thowa alikuwa akizungumza wakati wa kilele cha wiki ya Elimu na Mazingira ya manispaa hiyo, iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambako shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi zilishiriki na kutunukiwa zawadi ya vyeti, vikombe na vifaa vya usafi.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo iliyotanguliwa na maandamano yaliyopokelewa na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, Afisa Elimu (Sekondari), Violet Mlowosa, alisema maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujengea hamasa wanafunzi na walimu kufanya bidii kitaaluma na kutunza mazingira.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Zanaki, Salim Mgamba, alisema shule yake itaendelea 'kutesa' kitaaluma kwa sababu wazazi na walezi wanasaidia kila kinachohitajika, hivyo kuwarahisishia walimu na viongozi wa elimu manispaa hiyo kutimiza majukumu yake.
CHANZO: NIPASHE