Katika mkutano mkubwa uliofanyika muda mchache uliopita katika uwanja wa Moses Mabhida Stadium uliopo Durban, viongozi mbalimbali wa serikali, dini na chama cha Inkatha Freedom Party (IFP), walipanda jukwaani kujaribu kupunguza jazba za wananchi ambao wamekuwa wakiwasaka wageni katika nchi hiyo na kuwauwa na kuwajeruhi kwa madai kuwa wageni wananyang'anya nafasi zao za kazi. Kiongozi wa IFP Chief Buthelezi alichukua muda huo kutetea kauli ya Mfalme wa Wazulu Zwelithini ambaye ndie alisema 'Wageni lazima waondoke Afrika ya Kusini' sentensi inayodaiwa ndiyo iliyoanzisha wimbi hili la vurugu. Buthelezi alitetea kuwa Mfalme wao alikuwa ana maananisha kuwa muda umefika kwa wenyeji kukubali kufanya kazi ngumu.!!! Chief Buthelezi aliongezea katika mkutano huo kuwa, kufukuza wageni hakutasaidia kwani tatizo liko katika jamii yenyewe ya South Africa. Buthelezi alikumbusha kuwa historia ya Afrika ya Kusini inatambua jukumu lililochukuliwa na nchi nyingine za Afrika katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi. Na IFP imekubali kuwa fujo zinazoendelea zilianzia KwaZulu Natal na kuenea sehemu nyingine, lakini chama hicho kiliendelea kutetea kuwa matamko ya mfalme wao yalichukuliwa na wahuni kuanzisha vurugu. Kabla ya hapo katika mkutano huo uliokuwa na watu kama 6000, kiongozi mwingine wa Kwa Zulu Natala Senzo Mchunu aliyeomba wananchi wajitahidi kufuta doa chafu linaloongeza kuchafua jina la nchi yao, hapo ikaanza zomea zomea ilimfanya akatishe hotuba na kuondoka jukwaani. Baadhi ya wanachi wanasema watafanya lolote ambalo Mfalme wao ataamua
Habari hii na picha kwa hisani ya mtandao wa EYEWITNES NEWS