Monday, August 03, 2015

WAPIGA KURA WACHOMA MOTO BOKSI LA KURA



WAPIGA KURA WACHOMA MOTO BOKSI LA KURA

Wanachama 401 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), tawi la Gidamula, Kata ya Gidehababieg, wilayani Hanang, wamevamia kituo cha kupiga kura na kuchoma moto kura zilizokuwa kwenye boksi baada ya kuelezwa wasingeweza kupiga kura kwa vile namba za kadi zao hazimo kwenye daftari la wanachama.


 
Wakati wanachama hao wakichoma moto kura hizo, baadhi ya wanachama katika tawi la Orbesh lililopo Kata ya Ideti, walikuja juu na kulazimisha uchaguzi huo kusitishwa baada ya majina yao kutokuwepo kwenye daftari la wanachama licha ya kuwa na kadi za CCM.
 
Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang, Kajoro Vyohoroka, alithibitisha kuchomwa kwa kura katika tawi la Gidamula na kusitishwa upigaji kura tawi la Orbesh juzi.
 
Alisema baada ya kushauriana na Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, walikubaliana zoezi la kura lifanyike upya kwa siku ya jana.
 
Akifafanua zaidi kuhusu vurugu hizo, alisema, awali upigaji kura tawi la Gidamula ulianza vizuri asubuhi, lakini ilipofika majira ya saa 9 alasiri, liliibuka kundi kubwa la wanachama waliounga foleni wakitaka watumie haki yao ya kupiga kura licha ya namba za kadi zao kutokuwa katika daftari.
 
"Walikuwa na kadi halali, lakini wakati wakifanyiwa uhakiki kwenye daftari la wanachama katika tawi halikuonyesha namba za kadi hizo.
 
"Hali hiyo ilisababisha wanachama, wasimamizi na viongozi wa tawi na wagombea kugawanyika huku wakitaka waruhusiwe kupiga kura huku wengine wakipinga.
 
"Sasa wanachama hao wakaona haki yao ya kupiga kura itapotea…wakajiunga kwenye foleni huku wakisema kura haiwezi kuendelea kupigwa vinginevyo na wao waruhusiwe kupiga.
 
Hata hivyo, vurugu hizo zilisababisha wanachama hao kuvamia chumba cha kupigia kura na kubeba boksi la kuwekea kura na kutoka nalo nje na kuchoma moto kura zote kuharibu ushahidi.
 
"Mwanzoni walichukua boksi la kura huku wakidai haziwezi kuhesabiwa bila ya wao kuruhusiwa kupiga kura, lakini baadaye wakatoka nazo na kuzichoma moto ili kupoteza ushahidi kabisa.
 
Alisema walikuwa wakisema wanafanya hivyo kwa sababu wameona haki yao ya kupiga kura inapotea.
Walisema kosa lililotokea la kutoandikwa namba zao katika daftari hilo sio la kwao hivyo hawapaswi kuzuiwa kupiga kura.
 
"Niliwasiliana na Katibu wa Mkoa kuhusu suala hilo naye akaunga mkono kura zipigwe upya leo (jana)… baada ya kwenda kuwasikiliza na kutatua sintofahamu hiyo.
 
"Nimeitisha kikao cha halmashauri ya tawi, mabalozi wote katika tawi hilo na kamati ya siasa ya kata pamoja na wagombea," alisema na kuongeza, kikao kimefanyika vizuri na zinarudiwa kupigwa. Akizungumzia tukio la pili katika tawi la Orbesh, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Vyohoroka alisema, baadhi ya wanachama katika tawi hilo waliokuwa na kadi hawakukuta majina yao yameorodheshwa katika daftari la wanachama.
 
Alisema majira ya asubuhi wanachama ambao hawakukuta majina yao walipoelezwa kuwa hawawezi kupiga kura waliondoka bila matatizo, lakini ilipofika saa 9:45 wachache ambao hawakukuta majina yao walikataa kuondoka.
 
Alisema wanachama hao walitaka waruhusiwe kupiga kura hivyo wakalazimisha zoezi la kupiga kura lisitishwe.
 
Alisema katika hatua hiyo kulikuwa na mgawanyiko kati ya wasimamizi, viongozi wa tawi na wagombea ambapo baadhi yao walitaka waruhusiwe na wengine wakipinga.
 
Alisema waliopinga walitaka wale waliozuiwa majira ya asubuhi nao waitwe ili kupiga kura.
Alisema mtafaruku huo ukasababishe zoezi hilo liahirishwa hadi jana.
 
Alisema aliwenda kukutana na uongozi wa ngazi ya tawi hilo pamoja na wagombea ili kutatua tatizo hilo na kura zilipigwa upya kwa kuwaruhusu wale ambao majina yao hayakuwamo kwa sababu tatizo lililotokea lilikuwa la kifundi lililosababishwa na kati ya tawi kushindwa kuandika majina katika daftari hilo.
 
"Tatizo la Orbesh ni la taratibu za kiufundi…hili ni tawi jipya toka Ideti, hivyo wanachama hao walikuwa bado hawajahamishwa kutoka upande mmoja wa tawi kwenda tawi lingine.
 
"Taratibu za kiufundi tu…aliyehamisha majina kwenda Orbesh hakuhamisha majina yote na kuyapeleka kila upande.
 
"Nimeenda na kuyapitia madaftari ya pande zote na kuhakiki majina na hatimaye wamepiga kura," alisema.
 
Katika uchaguzi huo, Katibu wa CCM Wilaya, alisema mbunge aliyemaliza muda wake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Dk Mary Nagu, alikuwa anaongoza kwa kupata kura 21,837 katika matawi 148 kati ya matawi 150 yaliyopo jimboni humo.
 
Alisema matokeo ya kata mbili yalikuwa yakisubiriwa baada ya wananchi kurudia kupiga kura.
 
Wagombea wengine wa nafasi ya ubunge jimboni humo na kura zao katika mabano ni Peter Nyalandu (5,558), Wakili Duncan Mayomba (4,412) na Dk Eliamani Sedoyeka.
Kata mbili ambazo zilikuwa na vurugu zimerudia uchaguzi.

NIPASHE