Ripoti za hospitali nchini na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa baadhi ya wanawake hutoa mimba kwa njia zisizo salama, ambazo huharibu kizazi, kuwasababishia ugumba na wengine vifo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika zahanati na hospitali kubwa za wilaya jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa asilimia kubwa ya wanawake hutoa mimba mitaani kwa kutumia njia za kienyeji na wataalamu wasio na ujuzi. Baadhi ya njia zisizo salama ambazo hutumika ni spoku za baiskeli, utomvu wa mti wa muhogo, vyuma vyenye ncha kali na vidonge bila kufuata maelekezo ya madaktari.
Utomvu huo una sumu ya 'oxytocin' inayoweza kuharibu mimba na wengine hutumia vidonge vya "misoprostol" na "morning after" vyenye uwezo wa kuharibu mimba, ambavyo vinauzwa kiholela katika maduka mengi ya dawa.
Hospitali ya Temeke
Kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, zaidi ya wanawake 200 walifikishwa katika hospitali hiyo wakiwa na matatizo ya uzazi, huku 12 kati yao wakithibitika kujaribu kutoa mimba kienyeji.
Muuguzi Kiongozi wa Wodi ya Sita katika hospitali hiyo, Mwasi Mwasamaga alisema wanawake wengi wanaofikishwa hospitalini kutokana na kutoa mimba kiholela huwa katika hali mbaya.
"Pamoja na kuwa wanakuwa katika hali mbaya, mara nyingi hawasemi ukweli njia gani waliyotumia kutoa mimba, lakini sisi kwa utaalamu wetu huwa tunajua kuwa wametoa mimba," alisema.
Muuguzi Kiongozi, katika Jengo la Wazazi, Beatrice Temba alisema wanaofikishwa hospitalini hapo, wengine huwa wamepata maambukizi kwenye kizazi, maambukizi hayo huweza kuingia hadi katika mfumo wa damu na katika ogani zilizo karibu na kizazi. Alisema wanawake wanaotoa mimba kiholela huwa wanatolewa na watu wasiokuwa na ujuzi, wakati mwingine hupata madhara yanayosababisha kizazi kutolewa kabisa, kupungukiwa damu kwa kiasi kikubwa, maambukizi kwenye njia ya mkojo au kinga ya mwili kushuka na baadhi kufa.
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili wa mwaka 2012 kuhusu utoaji wa mimba uliofanywa katika kata za Wilaya ya Temeke umeonyesha kuwa asilimia 33 ya wasichana walipata mimba zisizotarajiwa. Kati yao, asilimia 26 walikiri kuzitoa na asilimia 87 zilitolewa kwa njia zisizo salama ikiwemo kutumia spoku za baiskeli, miti ya muhogo, vitu vyenye ncha kali na vidonge.
Katika utafiti huo uliofanywa na Dk Neemba Mamboleo, wasichana 454 wenye umri wa kati ya miaka 19-25 walihojiwa na kukiri kuwa walitoa mimba kwa msaada wa marafiki wa kiume, ndugu au wahudumu wa afya.
Kuhusu hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema utoaji wa mimba ni kosa la jinai lakini pia aliuhusisha na uzembe.
Sophia alisema elimu inatolewa kila mara kuhusu uzazi wa mpango huku njia za kuzuia mimba zikitolewa bure kwa watu wa rika zote hata kwa wanafunzi lakini watu hawazingatii.
"Chanzo kikubwa ni kuzikimbia njia za uzazi wa mpango, hawataki kutumia hizi njia kuna kondomu, vidonge, vijiti ambavyo maeneo mengine unavipata bure," alisema.
Muhimbili
Takwimu zilizopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinaonyesha kwamba mwaka 2010-11, walipatikana wagonjwa 35 walioharibika mji wa mimba kutokana na utoaji mimba.
Kadhalika, takwimu za Muhimbili zinaonyesha kuwa kati ya vifo 155 vya uzazi, 53 vilitokana na utoaji wa mimba. Kitaifa mimba 2,430,000 zilitolewa kiholela na asilimia 18 zilisababisha vifo.
Mwananyamala/ Amana
Katika Hospitali ya Mwananyamala, takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu wanawake 276 walifikishwa kutokana na kesi za utokaji mimba. Kwa upande wa Hospitali ya Amana, wanawake 168 walifikishwa kwa matatizo ya utoaji mimba na kati yao, 18 wazitoa kwa njia za kienyeji na walikuwa na maambukizi katika mfumo wa damu, kuoza kwa kizazi au kutoboka.
Kwa mujibu wa madaktari, wakunga na wauguzi katika hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana, zaidi ya nusu ya wanawake wanaofika hospitali wakidai mimba zimeharibika chanzo huwa ni wao kwamba wamezitoa kwa njia zisizo salama.
Muuguzi Mkunga wa wodi ya wazazi wa Hospitali ya Amana, Eva Manyinye alisema baada ya wanawake wengi kuhojiwa ili waweze kusaidiwa kwa urahisi hukiri kutoa mimba kwa kutumia vifaa, kunywa dawa aina ya misoprostol na wengine kwa kipande cha mti wa muhogo.
"Wakati mwingine wanakuja wanafunzi, tena wenye umri mdogo, wengine wanakuwa wameshaharibu kizazi kabisa," alisema.
Waharibu vizazi
Uchunguzi umeonyesha pia kwamba idadi kubwa ya wanawake wanaotoa mimba kiholela aghalabu hutoboka utumbo, huchana kizazi, kizazi kuoza na wengine kuharibu figo. Daktari wa Magonjwa ya Wanawake wa Hospitali ya CCBRT, Fatma Suleiman alizungumzia madhara ya utoaji mimba na kusema ni bora mwanamke anayetoa mimba asisubiri hali yake kuwa mbaya, bali afike hospitalini mapema ili apewe matibabu.
"Kwa kawaida sisi madaktari kazi yetu ni kuokoa maisha, hata kama amefanya kosa lakini akifika hapa lazima atibiwe. Kwa hiyo, waje watibiwe na waseme ukweli ni njia gani wametumia kutoa mimba, ili watibiwe," alisema
Dk Fatma alisema wanawake wengi siku hizi hutumia vidonge ambavyo huuzwa kiholela kwenye maduka ya dawa, lakini huvitumia vibaya kwa kuzidisha dozi au kutumia dozi ndogo hivyo kuwasababishia madhara makubwa, ikiwamo kuchanika kwa kizazi au kupoteza maisha.
"Wengi tuliowahudumia wanachanika kizazi au kile kidonge kinaua kiumbe, kiumbe kinashindwa kutoka mpaka kizazi kinaoza," alisema.
Hatari ya 'misoprostol'
"Hivi vidonge vya 'misoprostol' awali vilikuwa vinatumika kutibu vidonda vya tumbo na kuzuia kutoka kwa damu kwa mama aliyejifungua, lakini sasa wengi wanatumia isivyo," alisema daktari wa magonjwa ya wanawake wa Hospitali ya Mwananyamala, Taiba Haidar.
Dk Haidar alisema kwamba wanawake huvitumia vidonge hivyo kienyeji kwa kuviingiza ukeni au kunywa na matokeo yake wanatokwa damu kwa wingi lakini mimba yenyewe haitoki na kwamba idadi kubwa ya wanawake wanaotoa mimba hukataa kusema njia walizotumia hadi pale wanapokuwa mahututi.
"Wakifika hapa huwa wameharibika sana, wengine wanatoka mpaka usaha na wameoza," alisema
Kuhusu utomvu wa muhogo, Dk Haidar alieleza: "Ule utomvu wa muhogo una sumu hiyo ya Oxtoxin, kwa hiyo wakiweka ukeni ule mti unafungua njia ya kizazi na utomvu unaua kiumbe na mimba inaharibika," alisema.
Dk Haidar alisema njia nyingine ni seti ya kusafisha kizazi iitwayo MVA, ambayo kwa kawaida hutumika kusafisha mimba ya chini ya wiki 12. "Lakini wapo watu wasio wataalamu wanazinunua hizi na kuzifanyia biashara kwa kuwatoa wanawake mimba," alisema na akaiomba Serikali kuzuia uuzwaji kiholela wa dawa za misoprostol ili kupunguza utoaji wa mimba kienyeji.
Shirika la WHO
Ripoti ya WHO ya mwaka 2011, inaonyesha kuwa msichana mmoja kati ya wanne hutoa mimba kwa njia za kienyeji na kati ya mimba 210 milioni zinazopatikana kila mwaka, 46 milioni sawa na asilimia 22 hutolewa.
Kadhalika, WHO inaeleza kuwa mwanamke mmoja hufa kila baada ya dakika nane kutokana na matatizo ya utoaji mimba usio salama.
WHO inasema kuwa kati ya hizo, mimba 20 milioni hutolewa kwa njia zisizo salama na wanawake 70,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na utoaji wa mimba usio salama.
Utafiti mwingine uliofanywa nchini na Dk Rose Kipingili na wenzake wa Taasisi ya Afya ya Umma ya Copanhagen mwaka 2012, umeonyesha kuwa wanawake 751 mkoani Kagera na Manispaa ya Temeke walitoa mimba kwa njia za kienyeji.
Asilimia 42 ya wanawake walitoa kwa kutumia mizizi ya mitishamba, miti ya mihogo na majani ya chai huku asilimia 54 walitolewa na watu wasiokuwa na ujuzi.
Sababu za kutoa
Kwa mujibu wa madaktari waliohojiwa, miongoni mwa sababu za wanawake kutoa mimba ni masomo, kupata mimba katika umri mdogo, kupata mimba nje ya ndoa, kutokuwa tayari kulea mtoto, kuficha watu wasijue kuwa amewahi kufanya ngono, shinikizo kutoka kwa wanaume au kutotaka kuzaa mtoto kutokana na mimba iliyotungwa kwa kubakwa.
Baadhi ya wauguzi na wakunga walieleza hata wanawake walio katika ndoa hufikia hatua hiyo baada ya kupata mimba wakati wakiwa na watoto wadogo.
Wanasheria
Mwanasheria wa Chama cha Wanasheria Wanawake nchini (Tawla), Sima Bateyunga amesema ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni lazima zitafutwe mbinu namna ya kupunguza pia utoaji wa mimba usio salama kwani unahatarisha maisha ya mamilioni ya wanawake. Sima alisema ukosefu wa elimu unasababisha vijana wengi kupata mimba zisizotarajiwa na hivyo kujikuta wakitoa mimba hizo kwa njia zisizo salama na kuhatarisha maisha yao.
Ofisa Sheria wa Tawla, Julius Titus anasema bado kuna pengo kubwa kutokana na kukosekana kwa sheria moja inayoangalia afya ya uzazi.