Ikulu ya White house imesema kuwa mipango ya kulifunga gereza la Guantanamo Bay nchini Cuba imefikia awamu za mwisho. Rais Barack Obama anasemekana kupatia kipa umbele suala la gereza hilo tangu aingie madarakani mwaka wa 2009 lakini limekumbwa na vizuizi kadhaa.
Gereza hilo la Guantanamo, ambalo limepewa jina la umaarufu kuwa Gitmo - limekuwa likitumiwa na Marekani kuwazuilia wapiganaji kutoka vita vya Iraq na vya Afghanistan bila kufunguliwa mashtaka yoyote. Rais Obama alitoa agizo la kirais kufungwa kwa kituo hicho mara moja katika siku yake ya kwanza. Lakini baraza la Congress lilikataa kuwahamisha wafungwa wa huko kuwaleta nchini Marekani kutokana na hofu za kiusalama.
Baadhi ya wadadisi wanaamini kuwa Marekani ilifungua gereza hilo nje ya ardhi ya Marekani ili wanajeshi wake wapate fursa ya kutumia mbinu zilizopigwa marufuku katika ardhi yao za kuwahoji wafungwa.
Gereza hilo pia limekumbwa kwa miaka mingi na madai ya ukiukajji wa haki za binadamu, ambapo njia zilizotumika kuwahoji wafungwa zimekashifiwa kuwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Aidha wafungwa wengi wamedai kuteswa, kupigwa na hata kulazimishwa kukiri baadhi ya mashtaka.
Wafungwa kadhaa maejaribu kujitoa uhai kutokana na mateso wanayodai kupata huko. Wengine wamechukua hatua kama kususia kula kwa wiki kadhaa kama njia ya kulalamika hali duni ya kibinadamu katika gereza hilo.
Wengi tayari wamerejeshwa nchini mwao japo kunao baadhi ambao wanaaminiwa kuwa hatari zaidi na hivyo hawaja achiliwa.
Msemaji mmoja wa ikulu ya white house ameambia waandishi kuwa mipango ya kuwasafirisha wafungwa hao kwa njia salama imefikia awamu za mwisho na itawasilishwa kwa baraza la Congress, lakini hakutoa maelezo zaidi.