Toka kushoto, Kocha Remmy
Ngabo(ngumi), Kanali Pellegreen Mrope
(Afisa Ulinzi, Ubalozini), Kocha Zachariah Gwandu (riadha) na Amos
Msanjila(Afisa Mambo ya Nje Ubalozini, Daraja la Pili ).
Mwanahabari Frank Eyembe wa
Urban Pulse (katikati) akiwa na kocha wa kuogelea, Sheha Mohammed Ali na kocha
wa masumbwi, Remmy Ngabo katika tafrija ndogo kuwaaga wanamichezo wetu London.
Balozi wetu Peter Kallaghe
akiwa na wahudumu wa Olimpiki wasiolipwa mshahara, Lesley Shayler, Alison
Cochrane na Steve Wiseall. Wa kwanza kulia ni Balozi wa Rwanda, Uingereza
Mheshimiwa Ernest Rwamucyo.
Balozi wa Tanzania Uingereza,
Mheshimiwa Peter Kallaghe( wa nne aliyesimama nyuma toka kulia) akiwa na
wanamichezo, makocha, maofisa na wahudumu wa kujitolea Olimpiki. Kulia kwake ni
mkuu wa msafara, Bwana Hassan Jarufu na Balozi wa Rwanda, Mheshimiwa Ernest
Rwamucyo (wa kwanza kulia) nyumbani kwake alipowaalika kuwapongeza na kuwaaga
jana Jumatatu.Picha Zote na Freddy Macha
--
Balozi wa Tanzania Uingereza,
Mheshimiwa Peter Kallaghe amewapongeza wanamichezo wetu walioiwakilisha nchi
katika Olimpiki kwa nidhamu na kuwataka wasivunjike moyo kwani sio sisi tu
tuliokosa medali.
“Wanamichezo wetu wameonyesha
tabia bora kinyume na watu wa nchi nyingine waliofanya mambo ya aibu sana. Lazima
tuwapongeze kwa kufikia viwango na kuibeba bendera ya Tanzania,”alisema.
Akiongea katika tafrija ndogo
kuwaaga wanamichezo saba, maofisa na makocha wao, Balozi Kallaghe alisisitiza
kwamba tusiwalaumu wanamichezo kwa
kushindwa kwani kuna mataifa mengi yaliyokosa medali. Tafrija hiyo
ilihudhuhuriwa na maofisa wote wa Ubalozi, wanahabari London na Balozi wa Rwanda
Uingereza, mheshimiwa Ernest Rwamucyo.
Kitakwimu ni asili mia kumi
tu ya washiriki 10,500 waliocheza michezo 26 (toka mataifa 204) wakapata
medali.
“Kuna mataifa tajiri kama
Ujerumani, Australia na India ambayo hayakufanya vizuri na pia wenzetu Afrika
mfano Kenya na Ethiopia ambao hawakuridhika au kufikia nafasi waliyozoea miaka
iliyopita.”
Balozi aliitaja nchi ya
Wafilipino (Philippines) yenye watu 93 ambayo ilikuwa na wachezaji 11 na
haikuambulia kitu. Kidesturi toka 1936,
Wafilipino wamekuwa wakishinda medali katika mchezo wa ngumi.
“Lazima tujiulize maswali ili
kufanikiwa mashindano yajayo na kujitayarisha ndiyo msingi. Vipaji vingi vipo
Tanzania. Tujaribu kuangalia na
kujiuliza wapi vilipo vianzio vya kuendeleza michezo yetu kutoka ngazi za chini
maana uwezo wa kushinda tunao. ”
Akipigiwa makofi balozi
alimtaja mkimbiaji maarufu wa Uingereza mwenye asili ya Kisomali, Mohammed “Mo”
Farah aliyefanya vibaya sana Olimpiki ya 2008, China. “Baada ya kushindwa
kabisa Beijing, Mo Farah alijilaumu na kulia sana; ila hakuvunjika moyo;
alirudi akajiandaa vizuri na matokeo yake mwaka huu kashinda medali mbili za
dhahabu.”
Naye mkuu wa msafara Bwana Hassan Jarufu aliushukuru ubalozi wetu
Uingereza kwa ukaribisho mzuri uliohakikisha kwamba wanamichezo wako sawa toka
walipowasili hapa majuma mawili kabla ya Olimpiki. Aliwataja pia wasaidizi wenyeji wa Uingereza,
Alison Cochrane, Steve Wiseall na Lesley Shayler aliyewahi kuitembelea Bongo na
kuipenda sana.
“Hawa wamekuwa wenyeji wetu wazuri sana,”
alisema.
Bwana Jarufu alifahamisha kwamba
wanamichezo wetu shurti kupongezwa kwa kujitahidi kufanya shughuli hii bila
ajira au kazi maalum.
“Kwa mfano wakimbiaji wa mbio
za marathon wanatakiwa kiafya wakimbie mara nne tu kwa mwaka kusudi wawe tayari
kwa mashindano makubwa, lakini kutokana na kukosa ajira au msaada wa kifedha wanalazimika
kushindana mara nyingi zaidi ili waishi. Na si ajabu ukamsikia mmoja mmoja
akilalamika kashindwa mashindano makubwa kama Olimpiki kutokana na majeruhi
fulani mwilini.”
Katika michuano ya siku ya
mwisho Jumapili wanariadha watatu, Faustin Mussa, Samson Ramadhan na Mohammed
Msondiki Ikoki walishiriki mbio za marathon na hawakupata medali yeyote. Mshindi alitoka Uganda Stephen Kiprotich
akifuatiwa na Wakenya: Abel Kirui na Wilson Kiprotich.