Thursday, July 23, 2015

PONDA AKWAA KESI MBILI ZA UCHOCHEZI


PONDA AKWAA KESI MBILI ZA UCHOCHEZI
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro  Imemkuta na makosa mawili ya uchochezi ya kujibu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kislamu Tanzania, Shekh Ponda Issa Ponda.

 Kutokana na hali hiyo, Agosti 7, mwaka huu, imepanga kuanza kusikiliza utetezi wake.
Sheikh Ponda atajitetea dhidi ya makosa mawili kati ya matatu yaliyokuwa yakimkabili.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Mary Moyo, alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama imemuona mshtakiwa huyo ana kesi ya kujibu katika shtaka la pili na la tatu.
Alisema katika kosa la kwanza mahakama hiyo imeona Ponda ana kesi ya kujibu kwa kuwa shtaka hilo lilitolewa uamuzi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kutupa ombi lake la kufutiwa kesi hiyo hivi karibuni.
Alisema maamuzi yanayotolewa na Mahakama za juu hayawezi kupingwa na mahakama za chini yake.
  Alisema mahakama hiyo  imeridhika na ushaidi wa upande wa mashtaka ambao ulipeleka mashahidi, mkanda wa video uliorekodiwa katika eneo aambako mshtakiwa huyo alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi na nyaraka mbalimbali. 
 Wakili wa upande huo wa utetezi, Juma Nassoro, alikubaliana na uamuzi wa mahakama hiyo na kuahidi kuwasilisha mashahidi siku hiyo.
Kwa upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Sunday Hyera, uliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi kwa madai kuwa  Wakili Kiongozi wa Serikali, Bernard Kongola hakuwapo mahakamani kutokana na dharura.
Ponda alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Agosti 18, mwaka juzi na kusomewa mashtaka hayo matatu na Wakili Kiongozi wa Serikali, Bernard Kongola.
Kongola alidai kuwa Agosti 10, mwaka 2013 alitoa maneno ya uchochezi katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro kwa kuwaambia Waislamu wasikubali kuunda kwa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwa kuwa zimeundwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambao ni vibakara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali.
Aliendelea kudai kuwa Ponda aliwaambia Waislamu hao kuwa kama watajitokeza watu hao na kujitambulisha ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha ya msikiti na kuwashambulia kwa kipigo.
Alidai mshtakiwa huyo pia alikiuka amri ya Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka 2013 ya kumtaka  kuhubiri amani  ndani ya mwaka mmoja wakati akitumikia kifungo cha mwaka mmoja nje. 
Alidai Agosti 10, mwaka juzi  katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, Sheikh Ponda aliwaambia Waislamu kuwa serikali ilipeleka jeshi mkoani Mtwara kudhibiti vurugu zilizotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini haikufanya hivyo kwa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.
Alidai maneno hayo ni ya uchochezi kwa sababu yalikuwa yakiumiza imani za watu  wengine kinyume cha sheria. 
Kosa ambalo hatatakiwa kujitetea ni la kwanza kwa kuwa mahakama ilishatoa uamuzi.
Jana wafuasi wa Sheikh Ponda waliofika mahakamani hapo majira ya saa moja na baadhi yao  walizuiliwa  kuingia ndani ya mahakama hiyo na baada ya kuahirishwa kwake wafuasi hao walianza kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu.

NIPASHE