Monday, July 13, 2015

Walimu waikimbia shule yao BAADA YA kuingiliwa kimwili nyakati za usiku


Walimu waikimbia shule yao BAADA YA kuingiliwa kimwili nyakati za usiku
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, imeombwa kupeleka walimu katika Shule ya Msingi Nambaza baada ya baadhi ya walimu kudai kufanyiwa vitendo vya kishirikina kwa kuingiliwa kimwili nyakati za usiku na hivyo kusababisha kuikimbia shule hiyo.
 
Wakifunga kikao cha mwisho cha madiwani wa halmashauri hiyo mjini Bunda, baadhi ya madiwani akiwamo wa kata ya Nansimo, Sabatho Mafwimbo, alisema kutokana na walimu wawili wa Shule ya Msingi Nambaza kufanyiwa vitendo hivyo vya ushirikina, hivi sasa shule hiyo imepwaya walimu baada ya baadhi yao kukimbia.
 
"Mkurugenzi, tunaomba halmashauri yako ituletee walimu katika shule hiyo ili zitakapofunguliwa wanafunzi wafundishwe kuziba pengo la wale walioamua kukimbia," alisema Mafwimbo.
 
Alisema hivi karibuni walimu wawili wa kike wa shule hiyo, waliingiliwa ndani ya nyumba zao kwa njia zinazoadaiwa za kishirikina na kuwaingilia kimwili bila wenyewe kujitambua hali iliyowafedhehesha walimu hao.
 
Kufuatia tukio hilo, mwananchi mmoja aliuawa na wananchi wenye hasira kijijini hapo baada ya kutuhumiwa kuwa miongoni mwa 'wachawi' waliotenda ushirikina huo huku wengine saba wakazi wa kijiji hicho wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa mawili ya kupanga, kutenda kosa la ushirikina na kuwaingilia kimwili walimu hao.
 
Mwenyekiti wa Halmashauri, Joseph Marimbe, aliwataka wananchi wa kijiji hicho kuachana na vitendo vya ushirikina kwa sababu hali hiyo inasababisha walimu kuogopa kufundisha shule hiyo.