Monday, July 13, 2015

Dk. Slaa: Magufuli hafui dafu Ukawa



Dk. Slaa: Magufuli hafui dafu Ukawa
Katibu Mkuu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.

Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kimempitisha Dk. John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais  katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesema, mgombea huyo hana uwezo kukabiliana nao kwa kuwa hata jimboni kwake wamempita kwa idadi ya viti vya uongozi katika mitaa, vitongoji  na udiwani.
 
Katibu Mkuu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema Magufuli hawezi kushindana na Ukawa, kwani kwenye jimbo lake la Chato chama hicho kimechukua sehemu kubwa ya uongozi kuanzia ngazi ya mitaa na kata (udiwani).
 
Dk. Slaa alisema ikiwa kwenye jimbo lake mwenyewe Ukawa wamempita kwa nafasi hizo, hatakuwa na uwezo wa kushindana nao  katika nafasi hiyo ya juu kabisa nchini. 
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alipongeza mchakato wa mchujo uliofanywa na CCM katika kumpata mgombea.
 
Hata hivyo alisema Magufuli anahitaji msaada wa kidiplomasia kwani utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na wakati akiwa Rais.
 
"Walikuwa na mchakato mgumu kidogo hasa walipofikia kundi la watano, napongeza walipofikia. Huyo mgombea waliyempata, Watanzania wanamfahamu, ni mchapakazi…lakini utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na akiwa Rais…anahitaji msaada wa kidiplomasia," alisema Dk. Bisimba.
 
Mhadhiri mwandamizi wa  Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema  CCM hawajafanya makosa kumteua Magufuli kuwapeperushia bendera kwani ni mtu ambaye hajitambulishi kimakundi  huku akijipatia umaarufu katika utendaji na uchapaji wake wa kazi katika wizara ikiwamo ya Ujenzi.
 
Alisema, Magufuli ni mtu ambaye anafaa kukiwakilisha CCM kupambana na vyama vya upinzani kwani akiwa Waziri, wizara yake haina historia yoyote ya kashfa katika taarifa za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
 
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim, aliipongeza CCM kwa kufanikiwa kuvunja makundi yaliyokuwa yametawala kabla ya kupatikana kwa mgombea huyo. 
 
Alisema CCM kumpitisha Dk. Magufuli kumevunja makundi yote yaliyokuwamo, jambo ambalo halikutarajiwa.
"Ninaipongeza sana CCM kwa Mwenyezi Mungu, kuwaongoza kufanikiwa kuvunja makundi na kumchagua Dk. Magufuli, hii ni faida kwa chama na kwa Taifa pia," alisema.
 
Aliongeza:  "Ni bora walivyofanikiwa kumchagua Dk. Magufuli kuliko wangewachagua wagombea ambao walikuwa kwenye makundi,  yeye hana makundi  na hiyo itasaidia sana kwa chama na kwa taifa pia."
 
Kuhusiana na utendaji wake, alisema hana wasiwasi na yeye ni mtendaji mzuri na anaamini ataisaidaia Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Jamii kwa Madhehe