Wednesday, July 15, 2015

VYUO VYATAKIWA KUTOA ELIMU KULINGANA NA MAHITAJI YA AJIRA HAPA NCHINI



VYUO VYATAKIWA KUTOA ELIMU KULINGANA NA MAHITAJI YA AJIRA HAPA NCHINI
Na Woinde Shizza, Arusha
VIJANA wengi  wanaohitimu vyuo hawapati kazi mara tu ya kuhitimu

masomo yao kutokana na kutokuwepo kwa vyanzo vya ajira vinavyokwenda
sambamba na ongezeko la wahitimu na kuchangia kuwepo kwa wimbi la
wahitimu wasiokuwa na ajira nchini.

Hayo yalisemwa    na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na
utalii ,Selestini Gesimba alipokuwa akizungumza katika mahafali ya
tano ya Chuo cha Taifa cha Utalii(NCT) ,kampasi ya Arusha ambapo jumla
la wanafunzi 55  walihitimu fani za mapishi, uokaji,mapokezi,na huduma
ya vyakula na vinywaji katika ngazi ya cheti.

Alivitaka vyuo mbalimbali kutoa elimu kulingana na mahitaji ya ajira
ili kuwezesha wanafunzi wanaohitimu kupata ajira  kwa haraka na
hatimaye kuondokana na changamoto ya wimbi kubwa la wanafunzi
wanaohitimu na kukaa mtaani bila ajira.

Gesimba alitoa rai kwa vijana wa kitanzania kujiunga na Chuo cha Taifa
cha Utalii ili wapate ujuzi ambao utatoa fursa ya kufanya kazi kwenye
sekta ya utalii na pia fursa ya kuweza kujiajiri wenyewe.

'sekta ya utalii nchini ni ya muhimu sana na inapaswa kudhaminiwa
kwani imekuwa ikichangia asilimia 17.5 kwenye pato la Taifa na
kuifanya kuwa ya kwanza kwa kuingizia Taifa Dola bilioni mbili
ikifuatiwa na sekta ya madini ambayo imeliingizia Taifa Dola bilioni
1.7 mwaka 2004 .'alisema Gesimba.

Alisema kuwa, sekta hiyo ni miongoni mwa sekta inayokuwa kwa kasi
kubwa duniani ambapo imekuwa ikikua kwa  asilimia 4.5 hadi 5 kwa mwaka
ambapo imekuwa chachu ya kukuza na kuendeleza sekta nyingine za
kiuchumi kama kilimo, miundombinu , mawasiliano na usafiri pamoja na
kuwa kichochea kikubwa cha kupunguza umaskini katika jamii.

Naye Mtendaji Mkuu wa wakala wa chuo cha Taifa cha Utalii ,Rosada
Msoma alisema kuwa,chuo hicho kimekuwa kikijitahidi kutoa mafunzo na
kuwaunganisha wanafunzi wake na fursa mbalimbali za ajira ambapo kwa
mwaka huu kati ya wanafunzi hao 55 tayari wanafunzi 21 wameshapata
ajira huku wengine wakiendelea kuitwa kwenye usahili maeneo
mbalimbali.

Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake,Neema Mollel alisema
kuwa chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu
wa jenereta pindi umeme unapokatika chuoni hapo, ukosefu wa hostel
changamoto inayosababisha wanafunzi wanaosoma mbali kutoweza
kuhudhuria kozi mbalimbali chuoni hapo.

Aidha waliomba chuo hicho kuwezeshwa zaidi na kuweza kutoa kozi
mbalimbali kwa ngazi ya diploma ili kuwawezesha wanafunzi wake kupata
elimu ya juu zaidi ambapo itawawezesha kukabiliana na changamoto ya
ajira ndani na nje ya nchi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha ,Adoh  Mapunda alisema kuwa,serikali
mkoani Arusha wapo tayari kushirikiana na chuo hicho katika kuboresha
huduma mbalimbali za masomo ili kuwezesha chuo hicho kukua zaidi na
kuendelea kutoa elimu iliyo bora zaidi.

Mapunda alikitaka chuo hicho kuboresha zaidi maswala ya hoteli ili
kuwavutia wateja wengi zaidi kuweza kujiunga chuoni hapo kutokana na
elimu nzuri ,na kuwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri wa

kukitangaza chuo hicho ndani na nje ya nchi kwa ujumla.