Friday, July 31, 2015

Ndugai ahojiwa Polisi kwa kujeruhi mgombea.


Ndugai ahojiwa Polisi kwa kujeruhi mgombea.
ndugai
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai amehojiwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kumshambulia kwa fimbo na kumjeruhi mgombea mwenzake katika mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Kongwa kwa tiketi ya CCM, Dk. Joseph Chilongani.
Job-Ndugai
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, aliiambia NIPASHE mjini Dodoma jana kuwa walilazimika kumhoji Ndugai baada ya kupokea malalamiko kuhusiana na tukio hilo lililotokea wilayani Kongwa juzi.
Inadaiwa kuwa Ndugai alimpiga fimbo na kumjeruhi vibaya Chilongani wakati wagombea hao na wenzao watano wanaowania kuteuliwa kuwa wagombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM walipokuwa wakijinadi ili wapitishwe na wanachama wenzao jimboni humo.
"Tulipokea malalamiko, tumemhoji Ndugai na kisha tukamuachia kwa dhamana… hivi sasa tunaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo," alisema Kamanda Misime na kuongeza kuwa watatoa taarifa zaidi pindi uchunguzi ukikamilika.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya, alithibitisha vilevile kuwa Dk. Chilongani alipokewa kwao juzi jioni kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na kwamba hadi kufikia jana alikuwa bado akiendelea na matibatu.
"Anaendelea na matibabu lakini hali yake inaendelea vizuri," alisema Dk. Mpuya.
TUKIO LENYEWE
NIPASHE lilikwenda hadi Kongwa jana na kuzungumza na watu mbalimbali akiwamo Dk. Chilongani, ambaye alieleza yaliyomsibu huku mgombea mwingine ambaye pia ni Ofisa Biashara wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Simon Ngatunga, akisema ugomvi huo ulikuwa kati yake na Ndugai, kabla haujahamia kwa Dk. Chilongani.
Alisema kuwa juzi, wagombea wote saba walifanya kampeni katika kata tatu na kabla hawajamalizia ngwe hiyo, ndipo sakata hilo lilipozuka.
Aliongeza kuwa wakati wakimalizia kujinadi kwenye kata ya Ugogoni, yeye alipanda jukwaani kujinadi kabla ya kufuatiwa na Ndugai, kwa mujibu wa ratiba waliyopangiwa na kiongozi wa msafara huo.
Alisema Ndugai baada ya kupanda jukwaani, licha ya kunadi sera, alianza kumshambulia (Ngatunga), kwa maneno makali akimtuhumu kuwa amekuwa akishirikiana na watendaji wa halmashauri ya wilaya kufanya ubadhirifu.
"Aliposhuka jukwaani, akaendelea kunishambulia kwa maneno, nikamwambia kwa hadhi yako haustahili kufanya siasa za namna hii; akatishia kunipiga," alidai Ngatunga.
Kwa mujibu wa Ngatunga, ni wakati huo kibao kilipomgeukia Dk. Chilongani, kufuatia Ndugai kumtuhumu kuwa alikuwa akirekodi matukio hayo kwa kutumia simu yake ya kiganjani.
Alisema Ndugai kwa kutumia fimbo kubwa aliyokuwa nayo mkononi muda wote, alimpiga Ngatunga kwenye paji la uso na sehemu nyingine za mwili hadi akazimia.
Akizungumza na NIPASHE kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kongwa jana, baba mzazi wa Dk. Chilongani, Eliezer Chilongani, alisema baada ya kupatwa na kadhia hiyo, alipelekwa Kituo cha Polisi Kongwa kisha hospitali.
Naye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Kongwa, Lure Ndanshau, alilieleza NIPASHE jana hospitalini hapo kuwa walimpokea Dk. Chilongani juzi saa 12:00 jioni, akilalamika kuwa na maumivu makali kichwani.
Alisema baada ya kupatiwa huduma ya kwanza, uchunguzi wa kitabibu ulibaini haikuwa salama kuachwa arejee nyumbani, badala yake ikaamriwe abaki hospitalini hapo kwa uchunguzi na uangalizi zaidi.
"Asubuhi ya leo tukagundua hali yake ya shinikizo la damu ilikuwa juu, lakini kwa sasa tumefanikiwa kuidhibiti, anaendelea vizuri," alieleza Ndanshau.
Akizungumza na vyombo vya habari akiwa hospitalini hapo, Dk. Chilongani alielezea alichokumbuka kuhusu tukio hilo.
Alisema balaa hilo lilimpata juzi jioni akiwa kwenye kujinadi kwa wapigakura kuwania nafasi ya ubunge wa Jimbo la Kongwa kwa tiketi ya CCM.
"Nilikuwa nimekaa nikashuhudia hali ya kutoelewana kati ya Mheshimiwa (Ndugai) na mgombea mwenzetu Ngatunga, simu yangu nilikuwanayo mkononi na Mheshimiwa ni kawaida yake kuwa na fimbo mkononi, nikashtukia akinipiga na fimbo usoni," alidai Dk. Chilongani.
Kwa mujibu wa Dk. Chilingani, Ndugai alimtuhumu kwamba alikuwa akitumia kamera ya simu yake kumrekodi na kwamba pigo la mwisho alulokuwa akikumbuka ni la fimbo iliyotua kwenye paji lake la uso ma kusababisha aanguke chini.
Alisema tangu hapo hakuelewa tena kilichoendelea mpaka alipojikuta akipelekwa hospitalini huku akihisi kichwa kizito kikiwa na maumivu makali.
Juhudi za kumpata Ndugai kwa simu zake za kiganjani hazikuzaa matunda hadi tunakwenda mitamboni jana.
Hata hivyo, Kaimu Katibu wa CCM wilayani Kongwa, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi unaofanyika ndani ya chama hicho, Peter Minja, alilieleza NIPASHE kwamba taarifa walizonazo kuhusu tukio hilo, siyo rasmi, hivyo wanasubiri zikiwasilishwa na kufanyiwa kazi katika vikao vya ndani vya chama, zitatolewa ufafanuzi.
CHANZO: NIPASHE