Friday, July 31, 2015

UPELELEZI SAKATA LA NDUGAI KUMPIGA MGOMBEA LAKAMILIKA



UPELELEZI SAKATA LA NDUGAI KUMPIGA MGOMBEA LAKAMILIKA
 Job Ndugai
Polisi mkoani hapa wamekamilisha upelelezi wa tuhuma zinazomkabili Naibu Spika, Job Ndugai kumshambulia kwa fimbo kada mwenzake wanayewania kuteuliwa kuwania ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Kongwa, Dk Joseph Chilongani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema jana kuwa kinachosubiriwa ni ripoti ya daktari aliyemhudumia mgombea huyo ili kuendelea na hatua nyingine za kisheria.
Juzi jioni wagombea wenzake wengine wa ubunge jimbo hilo, walifika mjini hapa kwa lengo la kuzungumza na Kamanda Misime lakini walikwama na ilipofika saa mbili usiku, walitakiwa kwenda saa 3.00 usiku kuonana naye.
"Sisi tunashangaa mgombea huyu aliyefanya kitendo hiki bado yuko nje kwa hiyo tumeamua kuja kuonana na Kamanda wa mkoa ili waweze kuchukua hatua mapema," alisema mmoja wa wagombea hao, Simon Ngatunga.
Akizungumzia suala hilo Misime alisema walimkamata na kumhoji na aliachiwa baada ya kujidhamini mwenyewe.
Alisema jeshi la polisi linafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na halitamuonea mtu yeyote kutokana na fedha alizonazo au umaarufu, bali kazi itafanyika kwa weledi mkubwa.
Dk Chilongani aliyeruhusiwa jana kutoka hospitali ya Wilaya ya Kongwa alikokuwa amelazwa alisema:
"Hali yangu si nzuri sana kwa sababu presha si nzuri lakini kwa sababu jana (juzi) habari zilienezwa katika mitandao kwamba nimekufa ziliwashtusha watu na kuwafanya ndugu kumiminika kwa wingi, waliamua kuwaomba madaktari waniruhusu ili niendelee na matibabu nyumbani," alisema. Hata hivyo, alisema kutokana na hali yake kutorejea katika hali ya kawaida jana hakuweza kuhudhuria mkutano ya kujinadi uliokuwa ufanyike katika kata mbili.
"Kama CCM wakiniambia nilete malalamiko yangu kwa maandishi nitafanya hivyo lakini ninaomba haki itendeke, utaratibu wa sheria utafuatwa," alisema.
Alikanusha maelezo ya polisi kwamba yeye ndiye aliyekwenda kutoa maelezo polisi siku alipojeruhiwa na Ndugai... "Nilikuwa sijielewi ningewezaje kutoa taarifa ya tukio siku hiyo? Waliotoa taarifa ni ndugu zangu."
Ndugai anadaiwa kumshambulia Dk Chilongani kwa kumpiga ngumi na fimbo hadi kuzimia Jumanne iliyopita walipokuwa katika kampeni za kujinadi.