Wednesday, July 15, 2015

NCHI ZAIDI ZADHAMIRIA KUJIFUNZA KWA TANZANIA KUHUSU MATOKEO MAKUBWA SASHA (BRN)



NCHI ZAIDI ZADHAMIRIA KUJIFUNZA KWA TANZANIA KUHUSU MATOKEO MAKUBWA SASHA (BRN)
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar,Utawala Bora, Dk.Mwinyihaji Makame Mwadini akizungumza wakati akifunga mkutano wa Majadiliano ya Viongozi wa Jumuiya ya Madola ya Utawala Bora wa Afrika  uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.





Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia BRN, Bw. Omari Issa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa jumuiya ya Madola ya Utawala Bora Afrika katika Mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.






Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Omben Sefue akizungumza katika mkutano wa jumuiya ya Madola ya Utawala Bora Afrika katika Mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar,Utawala Bora ,Dk.Mwinyihaji Makame Mwadini  akiwa na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Madola ya Utawala Bora Afrika  katika picha ya pamoja katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
(Picha na Avila Kakingo,Globu ya Jamii)

MIAKA miwili tangu utekelezaji wa mfumo wa BRN uanze hapa nchini na kuonesha matokeo mazuri Katika kuboresha huduma za jamii, jumuiya za kimataifa na nchi kadhaa zimeanza kutamani kuja kujifunza. Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia BRN, Bw. Omari Issa, amesema kuwa inawezekana kufikia ufanisi wa juu katika utekelezaji wa huduma za jamii iwapo nchi nyingine zitauchukua mfumo wa utendaji wa BRN na kuutekeleza kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira na mahitaji yao.

"Sisi tulijifunza kutoka mfumo wa Malaysia uitwao Matokeo Makubwa ya Haraka (Big Fast Results) lakini tuliuoanisha na vipaumbele na mazingira yetu, kwani mahitaji yetu ni tofauti na kwao," alisema na kuongeza kuwa uwekaji wa vipaumbele, nidhamu ya utekelezaji na uwazi ni nguzo muhimu za BRN ambazo zinaweza kuigwa na kutekelezwa kwingineko duniani.

Akisisitizia kuhusu umuhimu wa uwekaji vipaumbele alisema nchi nyingi zinafanya makosa kwa kutaka kutekeleza kila kitu ili kupata mafanikio mengi kwa wakati mmoja. "Ni vyema kuanza na vipaumbele vichache na baadaye kueneza mafanikio na uzoefu huo kwa sekta nyingine," alisema Bw. Omari akiongeza kuwa: "Ni muhimu pia kupata ushirikiano na uelewa wa watumishi wa umma kwa sababu mfumo huu unahusisha kubadili fikra na utendaji ili wajielekeze katika kupata matokeo zaidi."

Aidha Bw. Issa alisisitiza kuhusu utayari wa PDB wa kuendelea kutoa uzoefu wake kuhusu utekelezaji wa BRN kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Madola. "Nafahamu kuwa changamoto ya utekelezaji ipo katika nchi nyingi kwa sasa; hivyo ni muhimu kwa nchi kujifunza kwa nchi nyingine kutokana na uzoefu walioupitia. Baadhi ya nchi zimekwisha tuma watendaji wao kuja kujifunza kutoka kwetu; na siku za karibuni tumepokea maombi mengi zaidi kutoka nchi jirani na hata kutoka nje ya Bara la Africa," alisema.