Wednesday, July 29, 2015

Mwigulu ahojiwa na Takukuru kwa rushwa


Mwigulu ahojiwa na Takukuru kwa rushwa
"Kuna baadhi walilalamika hadi kususia kampeni lakini tumesuluhishwa na tunaendelea na kampeni," 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Singida, inamhoji Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joshua Msuya alisema kwenye taarifa yake kwa umma na vyombo vya habari jana kuwa Mwigulu alianza kuhojiwa na Takukuru Wilaya ya Iramba kuanzia juzi na hadi jana alikuwa bado anaendelea kuhojiwa dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo, Mwigulu alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alisema Takukuru ilikuwa imeandaa kikao cha usuluhishi miongoni mwa wagombea wa vyama vyote baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka miongoni mwao.
"Kuna baadhi walilalamika hadi kususia kampeni lakini tumesuluhishwa na tunaendelea na kampeni," alisema.
Hivi karibuni wapinzani wa Mwigulu, David Jairo, Amon Gyuda na Juma Kilimba, walipeleka malalamiko Takukuru kuwa Mwigulu amekuwa akitoa ahadi za kuwapa wananchi wa jimbo lake pikipiki, baiskeli na kukarabati barabara kwa fedha zake katika kipindi cha kampeni, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za uchaguzi.
Msuya aliwatahadharisha wagombea wa udiwani na ubunge mkoani hapa kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye kampeni za kura za maoni na Uchaguzi mkuu.
Alisema watakaobainika kukiuka sheria hiyo kwa kutoa rushwa ya fedha taslimu, madawati, vifaa vya michezo au rushwa ya aina nyingine yoyote, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Takukuru Tanga yaonya
Uongozi wa Takukuru Mkoa wa Tanga, umedhamiria kuwabana wagombea ubunge na udiwani kutokana na malalamiko kwamba baadhi wamekuwa wakitoa rushwa.
Tayari taasisi hiyo imeanza kuwahoji baadhi ya wagombea wanaotuhumiwa huku ikifuatilia kwa siri michakato ya uchaguzi katika vyama vyote vya siasa pamoja na kutoa elimu ya Sheria namba 6 ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Aidano Ndomba alisema jana kuwa wagombea watambue kwamba taasisi hiyo ipo kazini na itawabana wote watakaobainika kutoa au kupokea rushwa.
"Tumeanza kuchukua hatua ya kuwahoji na kukusanya ushahidi kwa baadhi ya wagombea ambao wamelalamikiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa," alisema Ndomba na kusisitiza kuwa maofisa wa Takukuru wanafuatilia kwa siri michakato yote.