Wednesday, July 29, 2015

Mbunge wa CUF ahamia ACT



Mbunge wa CUF ahamia ACT
Amina Abdallah Amour

MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Amina Abdallah Amour amekihama chama hicho na kujiunga rasmi na ACT-Wazalendo.
Amour ambaye amehitimisha miaka 20 ya kuwa mwanasiasa ndani ya CUF, alikabidhiwa kadi ya chama hicho jana na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ramadhan Suleiman Ramadhani. Mbali na Amina pia chama hicho kimeeleza kuendelea kupokea wanachama mbalimbali visiwani humo kwa ajili ya kujiimarisha zaidi.
Hata hivyo Amour baada ya kukabidhiwa kadi yake alieleza kuwa wiki ijayo ataeleza bayana kilichomfanya kujiondoa ndani ya chama hicho. Aidha alisema, pia atazungumzia suala zima la kuingia katika makubaliano ya kumsimamisha mgombea mmoja wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) bila kuangalia mustakabali wa chama hicho kwa siku za baadaye.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Ramadhan alieleza kuwa katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakipokea wanachama wengi wanaojiunga na chama hicho. Alisema wananchi mapokezi ya wachama hao ni muendelezo wa ujenzi wa chama hicho nchini kote.