Thursday, July 30, 2015

‘Lipumba alikaidi amri ya polisi’NEW



'Lipumba alikaidi amri ya polisi'NEW
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba akiwa chini ya ulinzi wa polisi. 
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Sebastian Zacharia ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alimuomba Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba atii amri ya polisi ya kuzuia maandamano yao lakini alikaidi.
Zacharia ambaye alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke na kuhamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Upelelezi, alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Akitoa ushahidi, Zacharia alidai kuwa Januari 26, mwaka huu waliona tangazo la CUF kufanya maandamano na mkutano Januari 27, Mbagala Zakhem kupitia runinga ndipo alipowatuma watu wake wafuatilie kama kuna ukweli.
Alidai kuwa Januari 27, mwaka huu katika Mtaa wa Boko Temeke eneo hilo kipolisi lilikuwa chini yake.
"Sikuwa na taarifa ya maandishi niliwasiliana na Kamanda Simon Siro na kumwambia taarifa hizo za CUF kufanya maandamano na mkutano wanazo lakini wameyazuia na akaniletea nakala ya zuio hilo.
"Niliwaita maofisa wa polisi na kuwaonyesha nakala ya zuio, kisha nikataka wakae tayari kwa lolote litakalojitokeza.
Siku hiyo tulisubiri ili kuona kama kuna dalili zozote za maandamano, ilipofika saa saba mchana SP Msuya alinipigia simu na kunijulisha kuwa wameanza kukusanyika na Lipumba alikuwapo.
"Nikawataka waendelee kungalia kama wana dalili za kuondoka kwa maandamano," alieleza Zacharia.
Alidai kuwa wafuasi wa Lipumba waliendelea kuongezeka huku wengine wakiwa wameshika vipeperushi vya bendera za CUF na mabango.
"Baada ya nusu saa, Lipumba na wafuasi wake walianza kutoka Mtaa wa Boko na kuelekea Barabara ya Sudan hatimaye Mtongani... lilikuwa kundi la watu takribani 200," alisimulia na kuongeza:
"Niliwasihi wasifanye maandamano, watii zuio la polisi na kama hawajaridhika wakate rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini alikaidi."
Alidai kuwa Lipumba alikiri kupokea barua ya polisi ya zuio, lakini alimueleza kuwa kwa kuwa wamekwisha yaandaa wanaandamana.
Zacharia alidai kuwa alimsihi Lipumba tena atii katazo hilo la polisi hakufanya hivyo badala yake wafuasi wake waliwatukana polisi kuwa ni vibaraka wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
"Hata hivyo, walianza kuondoka na magari yao huku wafuasi wake waliyazunguka kwa mwendo wa mchakamchaka huku wakiwa wamebeba vipeperushi vya bendera za CUF na mabango kuelekea Mbagala Zakhem.
"Pia kulikuwapo na kelele, matusi huku watu wengine wakiendelea na shughuli zao hospitalini na benki ya NMB. Polisi tuliona siyo busara kwakuwa mazingira hayo ni hatarishi tukaenda eneo la Mtoni Mtongani kuwasubiri.
Walipofika katika eneo hilo walikuja, walipofika tulimuomba tena Lipumba ayasitishe maandamano, akasema anaenda kuongea na wananchi wake wanamsubiri Mbagala Zakhem.
"Tulitoa ilani mara tatu ili watawanyike baada ya muda tuliwakama watu 32. Polisi walitumia nguvu ya kawaida na tuliwapeleka kituo cha Kati," alidai Zacharia.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo.