Tuesday, June 30, 2015

TUNASUBIRI MIKAKATI MIPYA KUIOKOA SHILINGI



TUNASUBIRI MIKAKATI MIPYA KUIOKOA SHILINGI
Thamani ya Shilingi inazidi kuporomoka kadri siku zinavyokwenda na kusababisha bei za bidhaa mbalimbali kuendelea kupaa bila ya kuwapo na maelezo yoyote ya mkakati wa kudhibiti hali hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kipindi kinachoishia Aprili, thamani ya Shilingi iliporomoka hadi kufikia Sh1,815 kwa Dola 1 ya Marekani kulinganisha na Sh1,798.4 dhidi ya Dola moja kwa mwezi uliotangulia.
Maelezo ya kuporomoka huko kwa Shilingi yamekuwa ni mepesi tu kwamba Dola inazidi kuimarika kutokana na uchumi wa Marekani kuendelea kukua na pili ni nchi yetu kutouza bidhaa nyingi nje ya nchi na badala yake inaagiza bidhaa nyingi, hali inayofanya mahitaji ya Dola kuwa makubwa kuliko ya Shilingi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo za BoT, kiwango cha kuporomoka kwa thamani ya Shilingi kwa mwaka kilifikia asilimia 10.8 kutoka Sh1,637.7 kwa Dola moja ya Marekani ilivyokuwa Aprili mwaka jana.
Wakati thamani ya Shilingi ikizidi kuporomoka, bei za bidhaa zinazidi kuongezeka kiholela mitaani na sababu kubwa inayotolewa na wafanyabiashara imekuwa ni thamani ya Dola kuzidi kupaa. Hivi sasa, shati ambalo mwaka jana lilikuwa likiuzwa kwa Shilingi 30,000, sasa linauzwa kati ya Sh40,000 na 45,000.
Maelezo yamekuwa ni rahisi tu kwamba thamani ya Dola inazidi kupaa wakati Shilingi inazidi kwenda chini. Bei za vyakula sokoni zinazidi kwenda juu, licha ya takwimu kuonyesha kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kuonekana kuwa kidogo.
Tatizo kubwa tunaloliona kwa viongozi wetu ni kuridhika na maelezo hayo mawili kuwa kupanda kwa thamani ya Dola kunasababishwa na kukua kwa uchumi wa Marekani na nchi kununua bidhaa nyingi kutoka nje kulinganisha na zile inazonunua.
Haya ni maelezo mazuri lakini ambayo hayasaidii wananchi kuondokana na matatizo wanayoyapitia sasa.
Katika bajeti, kuna mikakati mingi ya muda mrefu ya kuimarisha thamani ya Shilingi ambayo mwananchi wa kawaida hawezi kunufaika nayo kwa wakati huu ambao anateseka kwa kupanda bei za vyakula na bidhaa mbalimbali.
Ada za shule na vyuo sasa zinapangwa kwa kutumia Dola kwa kuwa Shilingi inayumba, ada za pango za majengo ya ofisi, malazi, bei za huduma mahotelini na sehemu nyingi zote zinapangwa kwa kutumia dola, lakini kipato cha mwananchi hakipangwi kwa Dola na matokeo yake ni mlalahoi kuendelea kuumizwa na kuporomoka kwa thamani ya Shilingi.
Tunadhani Serikali inatakiwa ije na mpango kabambe wa muda mfupi wa kuhakikisha inakabiliana na suala hilo kwa sasa ili kuwapunguzia wananchi mzigo na pia kuja na mpango wa muda mrefu kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.
Kwa mujibu wa maoni ya wabunge wakati wa mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, kuna bidhaa nyingi zinazonunuliwa nje ya nchi ambazo zinapatikana au zinaweza kupatikana hapa nchini
Hili ni eneo ambalo linaweza kuangaliwa vizuri ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa bidhaa ambazo hazina umuhimu na zinaweza kupatikana hapa nchini.
Yapo maeneo mengine mengi ambayo yanatoa mianya ya fedha za kigeni kutumika bila ya sababu. Hivyo, Serikali ikidhibiti na kuibuka na mikakati mingine ya muda mrefu, mwananchi anaweza kupunguziwa mzigo anaoubeba sasa.
Kwa maana hiyo, tunashauri kuwa wakati mikakati ya muda mrefu ikiandaliwa, tuanze na wa muda mfupi.