Thursday, January 01, 2015

WEREMA APOKELEWA KWA FURAHA KIJIJINI KWAKE



WEREMA APOKELEWA KWA FURAHA KIJIJINI KWAKE

ALIYEKUWA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI JAJI FREDRICK WEREMA AMEPOKELEWA KIJIJINI KWAKE BAADA YA KUJIUZULU NAFASI HIYO HIVI KARIBUNI.
Jaji Werema amepokelewa kijijini kwake baada ya kujiuzulu nafasi hiyo hivi karibuni huku wananchi wa kijiji hicho wakiwataka watuhumiwa wote katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow kujiuzulu nafasi zao ili kulinusuru taifa kuingia katika mgawanyiko na machafuko ambayo wamedai yanaweza kuhatarisha amani.
Wakizungumza baada ya kumpokea Jaji Werema muda mfupi baada ya kuwasili katika kijiji hicho cha Kongoto tarafa ya Kiagata mkoani Mara, wananchi hao wamempongeza kiongozi huyo kwa kuchukua hatua ya kujiuzulu nafasi hiyo ya uanasheria mkuu wa serikali.
Wananchi hao pia wamesema ni jambo la busara kwa kiongozi wa umma kuchukua uamuzi kama huo katika kulinusuru taifa lake hasa baada ya kutuhumiwa katika sakata hilo.
Kwa upande wake Jaji Fredirick werema, akizungumza na wananchi hao amesema hawezi kuteteleka kwa uamuzi wake wa kujiuzulu huku akisema ni jambo la busara kama kiongozi wa umma unapohusishwa na tuhuma zozote kukubali kwa hiari yako kuwajibika ili kulinda maslahi ya taifa.
Kuhusu chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kushinda katika kijiji chake kwa nafasi ya uenyekiti wakihusisha ni kutokana na sakata la Escrow, Jaji Werema amesema hatua hiyo imetokana na wananchi kuchoshwa na baadhi ya viongozi wa CCM katika eneo hilo hivyo kuomba wananchi kumpa kiongozi huyo ushirikiano katika kutimiza wajibu wake.