JESHI la Polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limefanikiwa kukitambua kikundi cha mtandao wa kigaidi.
Kikundi hicho kinadaiwa kujihusisha na majaribio matatu ya kuwashambulia polisi, wakiwemo wa Kikosi cha Usalama Barabarani. Tayari, jeshi hilo linawashikilia baadhi ya watu wanaoshukiwa kuhusika na matukio hayo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema jana Jeshi lake limefanikiwa kumtambua mtuhumiwa aliyelipukiwa na bomu.
Pia, alisema jeshi hilo limebaini mtandao wote, unaojihusisha na matukio matatu ya kigaidi ya ulipuaji mabomu, yaliyolenga kushambulia askari Polisi yaliyotokea mkoani hapa.
Alisema, marehemu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa imebainika kuwa ni mzaliwa wa wilaya ya Tunduru, ambaye alizikwa Desemba 31 mwaka jana baada ya baba yake mzazi kujitokeza na kuzikwa Manispaa ya Songea.
Alisema, marehemu alikuwa ni miongoni mwa watuhumiwa wa kikundi cha kigaidi, ambapo tukio la kwanza wanatuhumiwa kuwarushia bomu polisi waliokuwa doria.
Bomu hilo lilitengenezwa kienyeji na lilitupwa Septemba 16 mwaka jana eneo la Mabatini. Mihayo alisema tukio la pili ni la Oktoba 27 mwaka jana, ambapo askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakiwa katika eneo la Mshangano, jirani na kituo cha kurushia matangazo cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) , wakiwa katika kazi zao za kawaida za ukaguzi wa magari, walitegeshewa bomu, ambalo baadaye liligunduliwa na askari hao na kufanikiwa kuteguliwa kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Alisema tukio la tatu ni la Desemba 25 mwaka jana wakati askari hao wakiwa doria katika eneo la Mtaa wa Majengo Kota, ambapo mtu huyo ambaye kwa sasa ni marehemu, akiwa na wenzake kadhaa, alirusha bomu hilo kwa lengo la kuwadhuru askari hao.
Lakini, kwa bahati lilimlipukia mrushaji na kumuua papo hapo kabla hajatimiza azma yake . Alifafanua kuwa katika matukio mawili ya Mabatini na Majengo, askari wanne walijeruhiwa kwa mabomu hayo.
Alisema mpaka sasa polisi inawashikilia watuhumiwa kadhaa na wengine wanaendelea kusakwa, ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.