Tuesday, January 06, 2015

MAGARI YA TANZANIA YAZUIWA KUCHUKUA WATALII JOMO KENYATTA


MAGARI YA TANZANIA YAZUIWA KUCHUKUA WATALII JOMO KENYATTA


Magari  yenye namba za usajili wa Tanzania zimepigwa marufuku na uongozi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya na kusababaisha adha kwa mamia ya watalii na Watanzania wengine ambao wanafika katika uwanja huo kuchukua wageni.

Amri hiyo ilitolewa tangu Desemba 22, mwaka jana baada ya askari wanaokagua magari  yanayoingia uwanjani hapo kuanza kuzuia magari yote  kutoka Tanzania kuingia wakidai kuwa wameagizwa na viongozi wao kufanya hivyo.

Wakizungumza na gazeti hili katika eneo la Astro lilipo geti la kwanza la kuingia uwanjani hapa, madereva wanaowapeleka watalii katika uwanja huo kutoka kampuni mbalimbali za kitalii, walisema hatua hiyo imewapa adha kubwa wageni hasa watalii ambao wengi walishangazwa kuzuiwa kuiingia katika uwanja huo wakiwa katika magari yanayotokaTanzania.

Ruben Kiondo, dereva wa kampuni ya Rainbow Shuttle. alisema anashangazwa na usumbufu wanaoendelea kupata hasa watalii wanaokuja nchini  Tanzania huku  serikali ikikaa kimya.

"Huwezi kuamini  lugha isiyo nzuri wanayojibiwa watalii wanaoelekea Tanzania kupitia uwanja huu  wakihoji askari wanaozuia magari ya Tanzania kuingia uwanjani, mara wanaambiwa kwanini msipande ndege huko uwanja wa Kilimanjaro,  tutawazuia msipite hata mpaka wa Namanga," alisema Kiondo.

Mfanyabiashara kutoka Arusha ambaye naye alifika katika lango la kuingilia uwaanjani hapoa juzi akiwa na gari dogo lenye namba za usajili za Tanzania,  Patel Bhatia,  alisema alifika katika uwanja huo kwa lengo la kuwachukua ndugu zake kutoka Uingereza, lakini alizuiwa  kuingia na kukaa nje hadi alipowasiliana na ndugu ambao walichukua teksi  kumfuata nje ya uzio  wa uwanja huo.

Mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji ya River Side inayobeba watalii wa ndani na nje,  Moses Kingori, alisema hatua hiyo imewaathiri kwa kiwango kikubwa kibiashara na kuleta hofu kubwa kwa watalii kutoaka Ulaya na Marekani.

"Habari hizi sasa zimeenea hasa katika sekta ya utalii, wageni wanaogopa sana, kitendo kinachofanywa  hakijawahi kushuhudiwa, wageni wanacheleweshwa kufika kwa wakati ndani ya uwanja tayari kupanda ndege hili ni jambo baya sana," alisema Moses.

Mkurugenzi wa kampuni ya Rainbow, Mathew Mollel, alisema wageni wanaotumia magari ya kampuni yake  wamepata usumbufu mkubwa sana toka zoezi hilo lianze.

Akizungumzia kuhusu hali hiyo, Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema hana taarifa rasmi za tukio hilo na kulaumu watendaji wa ngazi za chini katika serikali ya Kenya kwa kufanya vitendo vinavyotishia uhai wa Jumuia ya Afrika Mashariki.

"Ni vitendo ambavyo havikubaliki, sio sawa kabisa na vitaiangamiza Jumuiya ya Afrika Mashariki, hatukubali hata kidogo, kuna mengi yanayotokea  huko dhidi ya maslahi ya Tanzania na kwa kweli vinaweza kuiua jumuiya," alisema Sitta.

Alisema kuwa serikali ya Tanzania itachukua hatua haraka kufuatilia jambo hilo .

"Mimi na waziri mwenzangu wa jumuia upande wa Kenya tunatambua msimamo wa Rais wa Kenya kuhusu jumuia, lakini nina mashaka na watendendaji wa chini katika serikali na mamlaka kadhaa za Kenya zinaweza kuleta matatizo makubwa katika muungano wetu," alisema Sitta.
 
CHANZO: NIPASHE